• Jasusi mkubwa wa kike wa genge la Daesh ambaye pia ni kamanda, anaswa mjini Mosul

Jeshi la Iraq limefanikiwa kumtia mbaroni jasusi mkubwa wa kike aliyekuwa akitumika na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) mjini Mosul.

Gaidi huyo aliyetambulika kwa jina la Ahlam Muhsin Ali, mmoja wa wanachama wa ngazi ya juu wa kundi hilo la ukufurishaji ametiwa nguvuni katika operesheni iliyofanywa karibu na daraja linaloziunganisha pwani mbili za magharibi na mashariki mwa mji wa Mosul. Jeshi la Iraq limefafanua kuwa, Ahlam Muhsin Ali, aliyekuwa mmoja wa makamanda wa kike wa kundi hilo la ukufurishaji, amekiri kujishughulisha na ujasusi kwa miaka kadhaa kwa maslahi ya makundi ya kigaidi kabla na baada ya kuundwa kundi la Daesh dhidi ya serikali.

Sehemu ya magaidi wa kike wa kundi la Daesh

Kwa mujibu wa habari hiyo, gaidi huyo wa kike alianza kufanya ujasusi tangu utawala wa dikteta Saddam ulipoondolewa madarakani hapo mwaka 2003. Inaelezwa kuwa kabla ya kundi hilo la Daesh kufurushwa kutoka mjini Mosul, Ahlam Muhsin Ali alikuwa akikusanya majina na anwani za makazi ya askari na makamanda wa jeshi la Iraq kwa ajili ya kuwateka, kuwatesa na hatimaye kuwaua. Aidha amekiri kuwa baada ya kujiunga na genge hilo hapo mwaka 2014, alifanywa moja kwa moja kuwa mjumbe wa idara ya usalama na intelejensia ya Daesh huku akimlazimisha mume wake ambaye alikuwa polisi wa jeshi la Iraq, kujiunga na kundi hilo la ukufurishaji.

Baadhi ya wanawake wa Daesh waliokuwa wakifundishwa Uwahabi na Ahlam Muhsin Ali

Pia alikuwa na jukumu la kuwajaza fikra za kigaidi wanawake wa kundi hilo mjini Mosul na maeneo mengine ambayo yalikuwa yanadhibitiwa na genge hilo. Jeshi la Iraq limesisitiza kuwa, kupitia ujasusi wa mwanamke huyo , mamia ya raia wa kawaida wa mji wa Mosul wameuawa kwa namna ya kutisha na wengine wengi kuteswa vikali na wanachama wa Daesh (ISIS) kwa tuhuma za kushirikiana na serikali ya Iraq.

Jul 17, 2017 14:20 UTC
Maoni