Aug 11, 2017 07:08 UTC
  • Hatimaye UN yavunja kimya chake, yaitaka Saudia iheshimu haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeutaka utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia kukomesha jinai na mashambulio dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa nchi hiyo.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa, licha ya kuwa chombo hicho hakiwezi kuthibitisha ripoti za vyombo vya habari kuhusu jinai za Saudia huko al-Awamiya, lakini kingependa kuiona Riyadh inachukua hatua zisizokiuka haki za binadamu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waislamu hao wa madhehebu ya Shia waliutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati ili kukomesha mashambulio ya maafisa usalama wa Riyadh dhidi yao. Wakaazi wa al- Awamiyyah walizitaka taasisi za kimataifa na za kisheria kuunda tume ya kutafuta ukweli ili kuchunguza vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na utawala wa Aal Saud.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN

Katika miaka ya hivi karibuni, askari wa utawala wa kidikteta wa Aal-Saudi wameshadidisha mashambulizi kwa kutumia mizinga na silaha nyingine nzito katika makazi ya Waislamu wa Shia ya mji wa al-Awamiyah, mashariki mwa nchi hiyo.

Eneo la mashariki mwa Saudia limekuwa likishuhudia malalamiko ya wananchi wanaodai usawa tangu mwaka 2011. Hata hivyo badala ya utawala wa Aal-Saud kutekeleza matakwa ya wananchi, umekuwa ukitumia mkono wa chuma na ukatili kuwanyamazisha kwa nguvu wakazi wa mji wa al-Awamiyah. 

Tags

Maoni