• Saudia yakiri kutunguliwa ndege 10 za kivita za muungano vamizi nchini Yemen

Utawala wa Aal Saud umekiri kuwa ndege 10 za kivita zikiwemo nne za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala huo wa kifalme zimeanguka tangu ulipoanzishwa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen mwaka 2015.

Bila kuashiria jinsi ndege hizo 10 za kivita za muungano huo vamizi wa kijeshi zilivyoanguka, utawala wa Riyadh umekiri kuwa ndege tatu kati ya hizo ni za Saudia na zilizosalia ni za Imarati (UAE), Jordan, Bahrain na Morocco.

Wakati huohuo tovuti ya Yemeni Press imeripoti kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu umekiri kuwa Zaid bin Hamdan bin Zaid Al Nahyan, mwana wa kiume wa Rais wa zamani wa nchi hiyo amejeruhiwa katika ajali ya helikopta iliyotokea katika mkoa wa Shabwah kusini mashariki mwa Yemen.

Majeneza ya askari wa UAE waliouawa Yemen

Kamandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya Imarati imetangaza kupitia taarifa iliyotoa kwamba askari wanne wa jeshi la nchi hiyo waliuawa siku ya Ijumaa iliyopita  baada ya helikopta ya kijeshi kuanguka ilipojaribu kutua kwa dharura katika mkoa wa Shabwah kusini mashariki mwa Yemen.

Umoja wa Falme za Karabu unashirikiana na Saudia katika uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na utawala wa Aal Saud dhidi ya Yemen ambapo askari wa jeshi la nchi hiyo wanaendesha harakati zao katika eneo la kusini na kusini mashariki mwa ardhi ya Yemen.

Watu zaidi ya 40,000 wameuawa na kujeruhiwa nchini Yemen tangu Saudi Arabia ilipoanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu mwezi Machi mwaka 2015.../ 

Aug 13, 2017 08:10 UTC
Maoni