• Kuendelea huduma za Hashdu sh-Sha'abi, udharura wa operesheni iliyojengeka juu ya msingi wa sheria

Naibu Mkuu wa harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, Abu Mahdi al-Muhandis, amesema Jumamosi ya jana kwamba, Iraq ingali inaihitajia harakati hiyo kwani kukombolewa mji wa Mosul, hakumaanishi kuwa ndio mwisho wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).

Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi iliundwa na makundi tofauti ya Wairaqi kufuatia wito wa Ayatullah Sistani, Marjaa Mkubwa wa Waislamu wa Shia nchini humo baada ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kuudhibiti mji wa Mosul na kuutangaza kuwa makao makuu ya kile lilichokiita kuwa ni Dola la Khilafa hapo tarehe 10 Juni 2014. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na katika vita vya jeshi la Iraq dhidi ya magaidi, harakati hiyo ya wananchi imekuwa na nafasi chanya. Ni kwa ajili hiyo ndio maana tarehe 26 Novemba mwaka jana bunge la Iraq na kwa wingi wa kura likaitambua rasmi harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi kuwa sehemu ya jeshi la Iraq.

Abu Israel, mmoja wa wapiganaji shupavu wa Hashdu sh-Sha'abi 

Pamoja na hayo wapinzani wa harakati ya Hashdu sh-Sha'abi na licha ya kutambuliwa kwake kisheria, wamekuwa wakiendelea kuishinikiza serikali ya Baghdad iivunje harakati hiyo ambapo hadi sasa njama hizo zingali zinaendelea. Njama hizo za kuishinikiza serikali ya Iraq iivunje harakati hiyo zinatekelezwa kupitia fremu ya 'kuibua utata' na 'kubuni tuhuma'. Moja ya utata huo na tuhuma ambazo zimeibuliwa kuilenga harakati hiyo ni kwamba, Hashdu sh-Sha'abi imeundwa kwa madhumuni ya kushindana na jeshi la serikali. Tuhuma hizo zinazingatia kusambaratika kwa jeshi la nchi hiyo kulikotokana na vita vya mwaka 2003 kufuatia uvamizi wa Marekani, ingawa tuhuma hizo zimekuwa zikitupiliwa mbali kila mara na viongozi wa Iraq. Katika uwanja huo Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq amesisitiza kuwa, kamwe harakati tajwa haipo kwa lengo la kushindana na jeshi bali kinyume chake ni kwamba, jeshi, polisi na Hashdu sh-Sha'abi ni majeshi yenye kuhitajiana na yanayounda muhimili wa jeshi la taifa. Ukweli ni kwamba hatua ya kutambuliwa kisheria harakati hiyo kulikofanywa na bunge la Iraq haikuwa na lengo la kuilinganisha na jeshi, bali ilikuwa na lengo la kuimarisha zaidi uwezo wa jeshi la taifa hilo.

Wapiganaji wa harakati hiyo wakifanya mazoezi

Utata na tuhuma nyengine zinazotolewa kuilenga harakati hiyo hususan baada ya kukombolewa kwa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh (ISIS) ni hii kwamba, kwa kuzingatia tofauti zilizopo kati ya serikali na Hashdu sh-Sha'abi na makamanda wake, serikali imeamua kuivunja harakati hiyo ya wananchi. Sababu ya kutolewa tuhuma hizo pia ni kwamba, wapinzani wanadai kuwa harakati hiyo inakusudia kuwa kundi la kisiasa kwa ajili ya kuwatumikia baadhi ya shakhsia na makundi ambayo kimsingi ni wapinzani wa Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq. Tuhuma hizo zinatolewa katika hali ambayo muundo wa harakati hiyo ya wananchi iko chini ya uangalizi wa waziri mkuu mwenyewe, huku ikihesabiwa kuwa jeshi la wananchi la kusimamia usalama na ambalo halina malengo yoyote ya kisiasa. Kwa ajili hiyo inaonekana kwamba kuibuliwa tofauti kati ya waziri mkuu na harakati ya Hashdu sh-Sha'abi ni mchezo wenye lengo la kumshinikiza Haider al-Abadi aivunje harakati hiyo. Katika fremu hiyo Abu Mahdi al-Muhandis sambamba na kubainisha kwamba mahusiano ya harakati hiyo na serikali ya Baghdad ni mazuri sana, amesema kuwa, mahusiano ya Hashdu sh-Sha'abi na Waziri Mkuu ni mahusiano ya askari na kamanda wake.

Wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh 

Natija tunayoipata ni hii kwamba, wapinzani wa harakati hiyo ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi wanakusudia sambamba na kukamilika operesheni za kupambana na makundi ya kigaidi nchini Iraq, iwe pia mwisho wa uwepo wa harakati hiyo na kubakia kwake kusiwe na hadhi ya kutekeleza majukumu ya kiusalama na kuingia katika ulingo wa kisiasa. Hii ni katika hali ambayo kuendelea utendajikazi wa harakati hiyo kunategemea sababu mbili kuu muhimu: Mosi ni kutekeleza operesheni za kuyasafisha maeneo ambayo yanakaliwa na magaidi wa Daesh na pili ni kwamba kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na bunge la Iraq tarehe 26 Novemba mwaka jana, Hashdu sh-Sha'abi ni sehemu ya jeshi linalolinda usalama wa nchi, ambapo uwepo wake hauna ukomo wa muda maalumu.

Aug 13, 2017 12:17 UTC
Maoni