• HRW: Vikosi vya Saudia vimeuzingiria kikamilifu mji wa al-Awamiya

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limefichua kuwa vikosi vya usalama vya utawala wa kifalme wa Aal-Saud vimeuzingira kikamilifu mji wa al-Awamiya, ulioko mashariki mwa Saudi Arabia.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuna udharura wa vikosi vya usalama vya Saudia kusitisha mzingiro huo na kuruhusu bidhaa na huduma muhimu za kibinadamu katika mji huo sambamba na kuwaruhusu wakazi wake waingie na kutoka wanavyotaka.

Afisa huyo wa Human Rights Watch ameitaka serikali ya Riyadh iwawajibishe na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria maafisa usalama waliofanya mauaji ya raia katika mji huo kinyume cha sheria.

Shirika hilo limenukuu baadhi ya wakazi wa mji huo wakisema kuwa, huduma za umeme katika mji huo zimekatwa kwa kiasi kikubwa, huku zahanati na maduka yote ya dawa yakifungwa.

Maafisa usalama wa Saudia mjini al-Awamiya

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kupitia Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres,  kuvunja kimya chake na kuutaka utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia kukomesha jinai na mashambulio dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa nchi hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, askari wa utawala wa kidikteta wa Aal-Saud wameshadidisha mashambulizi kwa kutumia mizinga na silaha nyingine nzito katika makazi ya Waislamu wa Shia ya mji huo ambao umekuwa ukishuhudia malalamiko ya wananchi wanaodai usawa tangu mwaka 2011. 

Aug 13, 2017 13:46 UTC
Maoni