• Maelfu ya Wazayuni wasisitiza kuuzuliwa Benjamin Netanyahu

Maelfu ya Wazayuni wamefanya maandamano jirani na mji wa Tel Aviv Israel na kutoa wito wa kuuzuliwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu wakimtuhumu kwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz linaripoti kuwa, Wazayuni wapatao 3,000 wameandamana na kukusanyika mbele ya nyumba ya Avichai Mendelblit Mwanasheria Mkuu wa Israel. Waandamanaji hao wamemlalamikia Mwanasheria Mkuu huyo jinsi anavyoshughulikia faili la kesi ya ufisadi inayomkabili Benjamin Netanyahu.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kulaani vitendo vya ufisadi vya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Aidha waandamanaji hao wamemtuhumu Mwanasheria Mkuu wa utawala haramu wa Israel kwamba, ni mshirika wa Benjamin Netanyahu.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel

Waandamanaji hao wamemtaka Mwanasheria Mkuu wa Israel ajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, miji mingine ya Israel katika siku za hivi karibuni imekuwa ikishuhudia maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ambapo waandamanaji wamekuwa wakikosoa vikali siasa zake.

Netanyahu na mkewe wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya mashirika makubwa ya kibiashara na vilevile kufanya mazungumzo na Arnon Mozes, mchapishaji na mmiliki mwenza wa gazeti la Yediot Ahronoth ili atangaze habari zinazompendelea kwa lengo la kulidhoofisha jarida pinzani la Israel, la Hayom. 

Aug 13, 2017 14:20 UTC
Maoni