• Suluhisho la Marekani kwa mgogoro wa Qatar ni kushadidisha mgogoro huo

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Adel Al-Jubeir kuhusu mgogoro wa nchi yake na Qatar yanaashiria kuendelea kuwa mbaya mgogoro baina ya nchi hizi mbili za Ghuba ya Uajemi.

Akizungumza na waandishi habari Jumapili akiwa ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov  mjini Jeddah, al-Jubeir amesema: "Mgogoro wa Qatar unatokana na sera za uhasama za nchi hiyo dhidi ya nchi za eneo kwa kipindi cha miaka 20 sasa."

Al Jubeir kwa mara nyingine amedai kuwa, Qatar inapaswa kuacha kuunga mkono magaidi na kuwapa hifadhi watu wanaotafutwa na vyombo vya sheria. Pia amedai kuwa, Qatar inaingilia masuala ya ndani ya nchi zingine na hivyo inapaswa kuacha kufanya hivyo na kwamba ni wajibu itekeleze masharti 13 iliyopewa ili iweze kuwa na uhusiano mzuri tena na nchi za Kiarbau ambazo zimeisusia na kuiwekea vikwazo.

Ijumaa iliyopita, baada ya miezi mitatu ya mgogoro na mkwamo katika uhusiano wa Qatar na Saudi Arabia pamoja na Imarati, Bahrain na Misri, Sheikh Tamim  bin Hamad Al Thani, Amiri au mtawala wa Qatar alifanya mazungumzo ya simu na Mohammad Bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Wawili hao walizungumza kuhusu utatuzi wa mgogoro uliopo baina ya nchi hizo za Kiarabu. Lakini masaa kadhaa tu baada ya mazungumzo hayo, mgogoro mpya baina ya nchi hizo mbili ulianza.

Adel al Jubeir

Hii ni kwa sababu Kanali ya Televisheni ya Al Arabia na baadhi ya vyombo vya habari vya Saudia vimekuza kupita kiasi hatua ya Amir wa Qatar kumpigia simu Bin Salman na kusema nukta hiyo inaashiria kuwa Doha hatimaye imesalimu amri mbele ya watawala wa Riyadh. Baada ya hapo Shirika la Habari la Saudia SPA lilitoa taarifa na kusema kutokana na vyombo vya habari kupotosha habari kuhusu mazungumzo  hayo ya simu, mazungumzo yote baina ya Saudia na Qatar yanasimamishwa kwa muda.

Sababu ya hatua isiyotarajiwa ya Amiri wa Qatar kumpigia simu mrithi wa kiti cha ufalme Saudia, ni kufuatia jitihada za Marekani za kujaribu kutatua mgogoro baina ya madola hayo ya Kiarabu ambayo ni waitifaki wake.

Wiki iliopita, Rais Donald Trump wa Marekani alizungumza kwa simu na Sheikh Tamim Amir wa Qatar na kumtaka aongoze juhudi za kutatua mgogoro na Saudia.

Hii ni katika hali ambayo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Amir wa Qatar hakuwa tayari kuenda Marekani kuzungumza na wakuu wa nchi hiyo hata baada ya kualikwa.  Pamoja na hayo alikubali pendekezo la Trump la kumpigia simu mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Lakini jitihada hizo za Trump si tu kuwa hazikusaidia kutatua mgogoro uliopo bali zimefanya hali kuwa mbaya zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, Rais Trump wa Marekani na Mfalme Salman wa Saudia

Hapa tunaweza kutaja nukta mbili muhimu. Kwanza ni kuwa, kwa mtazamo wa Ikulu ya White House, si Saudi Arabia inayopaswa kuchukua hatua ya awali ya kutatua mgogoro na Qatar bali ni Qatar inayopaswa kuchukua hatua ya kutatua mgogoro uliopo. Pili ni kuwa, mazungumzo yoyote yanayofanyika pasina kuwepo hatua za kutatua mgogoro kimsingi hayawezi kuzaa matunda. Hii ni kwa sababu Qatar inataka Saudia iheshimu uhuru na mamlaka yake ya kujitawala. Lakini Saudia inataka Qatar iwe inatii na kutekeleza amri zote kutoka Riyadh. Ni kwa sababu hii ndio vyombo vya habari vya Saudia vikajaribu kueneza propaganda kuwa Amir wa Qatar amesalimu amri mbele ya watawala wa Riyadh.

Matamshi ya Adel al Jubeir yanaashiria kuwa pendekezo la Trump haliwezi kutatua mgogoro uliopo baina ya Qatar na madola manne ya Kiarabu yanayoongozwa na Saudia.

Sep 12, 2017 04:48 UTC
Maoni