• Waziri wa Vita wa Israel aota ndoto za alinacha kuhusu Hizbullah

Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa Israel itashinda katika vita vinavyoweza kutokea siku za usoni kati yake na harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kwamba katika vita hivyo wataisambaratisha moja kwa moja harakati hiyo ya muqawama.

Avigdor Lieberman ameyasema hayo baada ya kukagua manuva yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni ambapo amedai kwa mara nyengine tena kuwa vita vijavyo kati ya Israel na wapiganaji wa Hizbullah vitakuwa na tofauti kubwa kulinganisha na vita vilivyotangulia.

Wakati huohuo Reuven Rivlin, Rais wa utawala ghasibu wa Israel ambaye naye pia ametembelea luteka ya jeshi la utawala huo wa Kizayuni amesema mafunzo yanayotolewa hivi sasa kwa wanajeshi wa Israel ni kwa ajili ya kukabiliana na vitisho.

Wanamuqawama wa Hizbullah

Kutokana na kiwewe na kiherehere kilichoupata utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na nguvu za harakati ya muqawama ya Hizbullah, tangu wiki iliyopita wanajeshi wa utawala huo haramu wamekuwa wakifanya mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kushuhudiwa katika miongo miwili iliyopita huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya mazoezi ya kijeshi kila baada ya muda ili kwa dhana yake kutoa onyo na kuitunishia misuli harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon; lakini kila pale utawala huo vamizi ulipojaribu kufanya chokochoko dhidi ya Lebanon umekabiliwa na jibu kali la kipigo cha wanamapambano wa Hizbullah.../

Sep 13, 2017 14:58 UTC
Maoni