• HAMAS yatoa sharti la kuipatia Israel taarifa za askari wake iliowakamata mateka

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema itaupatia utawala wa Kizayuni wa Israel taarifa kuhusu askari wake waliokamatwa mateka katika Ukanda wa Gaza kwa sharti utawala huo haramu uwaachie huru kwanza Wapalestina 54 unaowashikilia kwenye jela zake.

Hassan Yusuf, Mbunge wa Hamas katika bunge la Palestina na afisa mwandamizi wa harakati hiyo amesema, kuanza mazungumzo ya mabadilishano mapya ya mateka na utawala wa Kizayuni kunategemea kuachiwa huru kwanza Wapalestina ambao waliachiliwa huru na Israel katika mabadilishano ya mwaka 2014 lakini baadaye utawala huo wa Kizayuni ukawakamata tena na kuwaweka gerezani.

Hassan Yusuf amesisitiza kuwa mara tu watakapoachiwa huru Wapalestina 54, mabadilishano ya taarifa baina ya Hamas na utawala wa Kizayuni yataanza mara moja; na harakati hiyo itatoa taarifa kuhusu hatima ya askari wa Israel waliokamatwa mateka katika Ukanda wa Gaza.

Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za Israel

Mbunge huyo wa Palestina amebainisha kuwa Muqawama ndio utakaokuwa mshindi katika mabadilishano yajayo ya mateka kwa sababu utawala wa Kizayuni utalazimika kulipa gharama na hauna njia nyengine isipokuwa kusalimu amri na kuyakubali masharti ya Muqawama. 

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imewakamata mateka askari wanne wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.../

Sep 13, 2017 14:59 UTC
Maoni