Sep 28, 2017 07:57 UTC
  • Sheikh Naeem Qassim: Kuwepo matakfiri katika Mashariki ya Kati ni mpango wa Kizayuni

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwepo matakfiri katika eneo la Mashariki ya Kati ni mpango wa kisiasa unaokamilisha mpango wa Wazayuni.

Sheikh Naeem Qassim ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya Al-Kawthar na kusisitiza kwamba magaidi wa kitakfiri wanatumia magari yaliyotegwa mabomu na kuzusha mtafaruku wa kisiasa kwa lengo la kusababisha machafuko na ukosefu wa amani ndani ya Lebanon. Ameongeza kuwa wakufurishaji hao walitaka kuuweka kwenye mashinikizo muqawama ili kuisaidia Israel katika uchokozi na uvamizi wake mpya dhidi ya Lebanon.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amebainisha kwamba Lebanon ilikuwa inakabiliwa na hatari kubwa lakini imewashinda matakfiri katika vita vilivyopiganwa katika maeneo ya Al-Qusair, Al-Qalamun, Arsal, Al-Qa'a, Ra's-Ba'alabyak na Al-Jarajirah.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh wakiwa nchini Syria

Kuhusiana na kuendelea kuwepo vikosi vya Hizbullah nchini Syria, Sheikh Naeem Qassem amesema, uwepo wa matakfiri hauishii kwenye suala la kijiografia bali ni harakati kamili ya kisiasa inayokamilisha uwepo wa utawala wa Kizayuni. Amesisitiza kwamba Hizbullah ilielekea Syria kwa madhumuni ya kupambana na makundi ya kigaidi na ukufurishaji na kusambaratisha mpango wa matakafiri na kuuhami muqawama; hivyo maadamu mgogoro ungalipo huko Syria, Hizbullah itaendelea kupambana nchini humo.../

Tags

Maoni