• Siku za kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq zaanza kuhesabika

Sambamba na ushindi wa kila siku wa jeshi la Iraq na makundi ya kujitolea ya wananchi katika mapambano ya kuliangamiza kundi la kigaidi la ِِِDaesh na kusafisha kabisa maeneo yote ya nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi ametangaza kuwa, kundi hilo litashindwa kikamilifu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mwaka 2014 kundi la kigaidi la Daesh likisaidiwa kwa fedha na silaha na Marekani na washirika wake hususan Saudi Arabia, lilivamia Iraq na kutwaa maeneo muhimu ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Tangu wakati huo wapiganaji wa kundi hilo wenye mitazamo na fikra za kiwahabi za mamufti wa Saudi Arabia, wamekuwa wakifanya jinai na mauaji ya kutisha. Uvamizi huo ulikabiliwa na mapambano ya jeshi la Iraq, makundi ya kujitolea ya wananchi na washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo yamefanikiwa kukomboa maeneo mengi yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu na kundi hilo. 

Al Hashdu al Shaabi

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi ametangaza habari ya kukaribia kusafishwa kabisa wanachama wa kundi la Daesh nchini humo wakati jeshi la Iraq likisisitiza kuwa, limekamilisha operesheni ya kukomboa eneo la al-Hawija huko magharibi mwa mji wa Kirkuku. Ukombozi wa eneo hilo ni ukurasa mwingine wa dhahabu  na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya kundi hilo la kigaidi. Ushirikiano mkubwa wa jeshi la Iraq na makundi ya kujitolea ya wananchi ni miongoni mwa sababu muhimu zilizopelekea kudhoofika sana kundi la kigaidi la Daesh licha ya kupata misaada ya hali na mali kutoka kwa serikali ya Marekani, Saudi Arabia na washirika wao. Ni kwa kutilia maanani ushirikiano huo ndiyo maana maafisa wa serikali ya Iraq wakautaja mwaka huu wa 2017 kuwa ni mwaka wa kifo cha kundi la kigaidi la Daesh nchini humo. Kukaribia kuangamizwa kikamilifu kundi hilo pia kunasadikisha bishara hiyo njema ya maafisa wa serikali ya Iraq. 

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi

Katika upande mwingine, kushindwa kwa magaidi wa kiwahabi wa Daesh katika nchi za Iraq na Syria ni kushindwa njama za madola ya kibeberu ya Magharibi na washirika wao ambao walitaka kutekeleza mipango yao ya kuzigawa nchi za eneo hili kwa kuliimarisha kundi hilo katika Mashariki ya Kati. Ukombozi wa eneo la al-Hawija pia unatambuliwa kuwa ni hatua muhimu ya kuzuia harakati za kutaka kujitenga nchini Iraq. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ukombozi huo unafunga njia ya kuingia wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga na kuunganishwa eneo hilo la lile la Kurdistan.

Kwa sasa na kutokana na kukaribia kuangamizwa kabisa kundi la Daesh nchini Iraq, Wamarekani na washirika wao ambao wanaona stratijia yao ikiyoyoma wanafanya mikakati ya kuanzisha njama mpya kwa shabaha ya kutimiza malengo yao nchini Iraq katika kipindi cha baada ya Daesh. Baadhi ya wachambuzi pia wanazitambua harakati za kutaka kujitenga eneo la Kurdistan na kura ya maoni iliyoitishwa katika eneo hilo kuwa ni sehemu ya njama hizo mpya za Marekani na washirika wake.

Bendera ya utawala haramu wa Israel ikipeperushwa katika maeneo yanayotaka kujitenga ya Kurdistan!

Serikali ya Iraq kwa upande wake imeng'amua njama hizo na kuchukua hatua za kisheria za kukabiliana na mipango inayokusudia kipindi cha Iraq baada ya Daesh. Mafanikio ya kisiasa na kijeshi ya Iraq dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh yamezidisha azma ya serikali ya Baghdad ya kukabiliana na njama na changamoto nyingine zinazoikabili nchi hiyo.  

Oct 12, 2017 02:46 UTC
Maoni