• Mkakati wa Israel wa

Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel Avigdor Lieberman, amesema vita vijavyo itakavyopigana Israel vitakuwa vya kukabiliana na kambi mbili za Hamas na Hizbullah kwa wakati mmoja na kudai kwamba jeshi la Lebanon limemezwa kikamilifu na Hizbullah na linaongozwa na harakati hiyo ya muqawama.

Matamshi ya Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni yametolewa pia na baadhi ya wachambuzi  na hata wanafikra wa Israel kama Uri Bar-Joseph ambaye anaitakidi kuwa vita na Hizbullah vitasababisha maafa na uharibifu ambao haujawahi kutokea katika mji wa Tel Aviv na wa kiwango hata kisichoweza kutasawarika. Ijapokuwa Hizbullah ya Lebanon ni imara zaidi na ina nguvu kubwa zaidi hivi sasa kuliko ilivyowahi kuwa katika wakati wowote ule lakini matamshi hayo yanayofanana yanadhihirisha kuwa Israel imeamua kutumia mbinu na mkakati wa "uenezaji hofu kuhusu Hizbullah".

Avigdor Lieberman (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al Jubeir, ambayo ni muitifaki wa Israel 

Kwa nini utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya kila uwezalo kueneza hofu juu ya Hizbullah? Jibu ni kwamba utawala huo haramu una malengo kadhaa unayofuatilia. La kwanza ni kutaka ianzishwe duru mpya ya hatua za kuiadhibu harakati hiyo ya muqawama hususuan kupitia serikali ya Marekani. Kuhusiana na suala hilo kuna taarifa mbalimbali kwamba serikali ya Donald Trump inataka kuiwekea vikwazo vipya Hizbullah ili kuishinikiza harakati hiyo ya muqawama na muitifaki wake muhimu zaidi, yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Gazeti la mtandaoni la Al Akhbar la Lebanon limeandika katika uchambuzi wake kuwa mhimili wa uovu unaoundwa na Marekani, Saudi Arabia na Israel umeratibu mpango wa vipengele vitano dhidi ya Hizbullah ambapo mzingiro wa kifedha ni sehemu ya tano ya mpango huo. Al Akhbar limeongeza kuwa "Rais Donald Trump wa Marekani anaharakisha kupitisha sheria ya vikwazo vipya dhidi ya Hizbullah; na lengo lake ni kutoa mashinikizo mapya dhidi ya Hizbullah".

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon

Lengo la pili la utawala wa Kizayuni ni kutaka kulichochea jeshi la Lebanon dhidi ya harakati hiyo ya muqawama. Huko nyuma kulikuwa na hitilafu na tofauti kati ya jeshi na harakati ya Hizbullah na hata baadhi ya mirengo ya ndani ya Lebanon ilikuwa ikipinga harakati hiyo ya muqawama kujizatiti kwa silaha; lakini hitilafu hizo hivi sasa zimepungua sana. Kwa kutoa matamshi hayo ya kichochezi yakiwemo ya Lieberman kwamba jeshi la Lebanon limeunganishwa na Hizbullah, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanataka kuzifufua tena hitilafu hizo za huko nyuma. Ufufuaji wa hitilafu hizo unafanyika pia kwa madhumuni ya kuibua tena mkwamo wa kisiasa ndani ya Lebanon kwa sababu mwaka ujao wa 2018 nchi hiyo inapaswa kuitisha uchaguzi wa bunge. Utawala haramu wa Israel unajaribu kwa upande mmoja kuichonganisha Hizbullah na makundi mengine ya kisiasa ya Lebanon ili kuvuruga mchakato wa uchaguzi ujao wa bunge; na kwa upande mwengine, kwa kushirikiana na muitifaki wake Saudi Arabia unataka kupunguza nguvu za kisiasa za Hizbullah katika bunge lijalo la Lebanon. Kupunguza nafasi na satua ya kisiasa ya Hizbullah ndani ya Lebanon nalo pia ni lengo jengine muhimu linalofuatiliwa na utawala wa Kizayuni kupitia mkakati wake wa kueneza hofu kuhusiana na harakati hiyo ya muqawama.

Rais Bashar al Assad wa Syria (kulia) na Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah

Kuna maudhui nyengine pia katika kadhia hii, nayo ni kwamba Israel haiko radhi kuona Bashar Al-Assad anabakia katika nafasi ya juu kabisa ya mfumo wa kisiasa wa Syria na kuendelea kulindwa umoja wa ardhi ya nchi hiyo kwa mssada wa waitifaki wa serikali ya Damascus ikiwemo Hizbullah. Hivi sasa utawala huo haramu unalikuza suala la nguvu na uwezo wa kijeshi wa Hizbullah ili kuwatia kiherehere watawala wa nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia kwa sababu Hizbullah ni mmoja wa waitifaki muhimu zaidi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo; na kuwa na nguvu kubwa harakati hiyo ya muqawama maana yake ni kuongezeka nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa utawala haramu wa Israel unatekeleza mkakati wa kueneza hofu kuhusiana na Hizbullah ili kuimarisha pia uhusiano wake na nchi za Kiarabu.../   

Oct 12, 2017 06:59 UTC
Maoni