• Idadi ya waliouawa katika shambulio la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Syria yafikia 65

Idadi ya waliouawa katika shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh katika mji wa Al Hasakah nchini Syria imefikia watu 65.

Magari mawili yaliyotegwa mabomu jana yaliripuka katika eneo la Abu Fas karibu na mpaka wa pamoja wa mikoa miwili ya Deir ez-Zor na Al Hasakah. Sambamba na shambulio hilo, magaidi wawili waliojifunga mada za miripuko walijiripua katikati ya umati wa wakimbizi wa Syria katika eneo hilo na kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa. 

Awali iliripotiwa kuwa watu 50 wameuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS)

Wengi kati ya waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi ni wakimbizi wanawake na watoto wanaohofia maisha yao, ambao waliamua kuyahama maeneo yenye machafuko ya Deir ez-Zor mashariki mwa Syria na kukimbilia maeneo yenye usalama kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Baada ya kupata vipigo vikali na kushindwa mtawalia kwenye medani za vita katika nchi za Iraq na Syria, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) sasa limeamua tena kutekeleza mkakati wa hujuma na mashambulio ya kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia.../ 

Tags

Oct 13, 2017 07:35 UTC
Maoni