• Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Waarabu zakaribisha mapatano ya Wapalestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamekaribisha mwafaka wa maridhiano yaliyofikiwa nchini Misri kati ya makundi ya Kipalestina ya HAMAS na Fat'h.

Taarifa ya ofisi ya habari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres imeeleza kuwa, katika mazungumzo ya simu aliyofanya Guterres na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Katibu Mkuu huyo wa UN ameeleza kufurahishwa na hatua zilizopigwa hivi karibuni katika mazungumzo ya mapatano ya kitaifa baina ya Hamas na Fat'h ambayo yataiwezesha serikali ya Palestina kutekeleza majukumu yake katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa mtazamo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuna udharura pia wa kushughulikiwa hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza hususan ya tatizo la umeme na utoaji huduma.

Viongozi wa Hamas na Fat'h baada ya kusaini mwafaka wa Cairo

Wakati huohuo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nayo pia imetoa taarifa ikikaribisha mapatano yaliyofikiwa mjini Cairo kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na ile ya Fat'h chini ya upatanishi wa serikali ya Misri na kueleza matumaini yake kuwa mapatano hayo yatawezesha kufikiwa malengo ya wananchi wa Palestina, kujitawala kwao na kuhitimishwa ukaliaji wa mabavu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi yao.

Jana Alkhamisi, harakati za Hamas na Fat'h zilisaini makubaliano ya maridhiano ya kitaifa kwa lengo la kuhitimisha utengano wa muda wa muongo mmoja uliokuwepo kati yao na kuainisha muda wa miezi miwili wa kutatuliwa matatizo yaliyopo.

Hayo yamejiri katika hali ambayo Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ametoa masharti manne ya kuyatambua rasmi makubaliano hayo ikiwemo kupokonywa silaha harakati ya Hamas, kusitishwa uchimbaji njia za chini kwa chini na uundaji makombora pamoja na kuachiwa huru askari wa Kizayuni waliokamatwa mateka katika Ukanda wa Gaza.../ 

Oct 13, 2017 07:35 UTC
Maoni