• Imarati ilitaka kuivamia kijeshi Qatar kwa kutumia mamluki wa US

Imebainika kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulikula njama ya kuishambulia kijeshi Qatar, kwa kutumia maelfu ya mamluki waliopata mafunzo ya kijeshi kutoka kampuni moja ya Marekani.

Abdullah bin Hamad al-Attiyah, Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar ameliambia gazeti la Uhispania la ABC kuwa, Imarati ilikodisha kampuni binafsi ya usalama ya Marekani iliyojulikana kama "Blackwater-linked" ambayo kwa sasa inafahamika kama Academi, kwa lengo la kuwapa mafunzo mamluki ambao wangetumwa katika operesheni ya kijeshi ya kuivamia Qatar.

Bin Hamad al-Attiyah amesema lengo la Imarati kuwapa mamluki hao mafunzo ya kijeshi lilikuwa ni kuivamia kijeshi nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi na kumuondoa mamlakani kwa nguvu Amir wake, lakini ilishindwa kupata uungaji mkono wa Washington.

Duru za habari zimeliambia gazeti la ABC kuwa, mamluki hao wa Imarati wamekuwa wakipokea mafunzo hayo ya kijeshi katika kambi ya Liwa Oasis mjini Abu Dhabi. 

Amir wa Qatar, Tamim Bin Hamad al-Thani

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe 5 Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi nyingine za Ghuba.

Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar mzingiro wa kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima.

Qatar inakadhibisha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Saudia.

Tags

Oct 15, 2017 07:50 UTC
Maoni