• Wairaq washerehekea kufurushwa Wakurdi kutoka Kirkuk, al-Abad aamuru kupeperushwa bendera ya Iraq

Wakazi wa mji wa Kirkuk nchini Iraq wamemiminika katika barabara za mji huo kushangilia ushindi wa jeshi la serikali kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi kwa hatua ya kuwafurusha wapiganaji wa Kikurdi mjini hapo na kisha kudhibiti hali ya mambo.

Hayo yamekuja baada ya jeshi la Iraq Jumatatu ya leo kuvamia mji huo na kuudhibiti huku wapiganaji wa Kikurdi wakilazimika kuondoka mjini hapo. Awali serikali yenye mamlaka ya ndani ya eneo la Kurdistan, ilikuwa imetangaza kuudhibiti mji huo sambamba na kudai kuwa, eti Kirkuk ni sehemu ya ardhi ya Kurdistan, huku ikiongeza idadi ya askari wake katika eneo hilo.

Bendera ya Iraq ikipandishwa mjini Kikrkuk baada ya kudhibitiwa na jeshi la serikali

Katika hatua nyingine ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abad imetangaza amri kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook ikiwa ni saa chache tangu kudhibitiwa na jeshi la serikali kuu ya Baghdad mji wa Kirkuk, ya kupeperushwa bendera ya Iraq katika maeneo yote ya mji huo. Baada ya amri hiyo, askari wa serikali, wameonekana wakipanda katika majengo ya serikali ya mji huo na kupeperusha bendera ya taifa hilo la Kiarabu. Habari pia zinaeleza kudhibitiwa na jeshi la nchi hiyo uwanja na kambi ya kijeshi ya al-Huriyyah katika mji huo wa Kirkuk. Kufuatia mafanikio hayo ya serikali kuu ya Baghdad, Masoud Barzani, kiongozi mkuu wa eneo la Kurdistan ya Iraq ameitaja hatua ya kuingia askari hao kuwa isiyostahiki na kuifananisha na uingiaji wa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika mji huo.

Masoud Barzani, kiongozi mkuu wa eneo la Kurdistan ya Iraq, ambaye anaonekana kushindwa njama za kuigawa Iraq

Kudhibitiwa na serikali ya Iraq mji wa Kirkuk ni pigo kubwa kwa viongozi wa Kurdistan na washirika wao, yaani utawala haramu wa Israel na Marekani. Inafaa kuashiria kuwa, viongozi wa Kurdistan na bila kuheshimu katiba ya Iraq waliitisha kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo tajwa, suala ambalo lililaaniwa vikali na serikali ya Iraq na hata nchi majirani na taifa hilo la Kiarabu. Utawala wa Kizayuni unahusika moja kwa moja katika kuwachochea viongozi wa Kikurdi wa eneo la Kurdistan kutaka kuigawa Iraq na kuanzisha utawala mwengine wa Kizayuni katika eneo.

 

Tags

Oct 16, 2017 16:37 UTC
Maoni