• Israel yaendelea kuwasaida magaidi wanaopumua pumzi za mwisho Syria, yashambulia jeshi la serikali

Katika kuendelea uungaji mkono wa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji yanayotaka kuiangusha serikali halali ya Syria, kwa mara nyingine jeshi la utawala haramu wa Kizayuni limeshambulia maeneo ya jeshi la Syria katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa, jeshi la Israel limeshambulia maeneo ya jeshi la serikali ya Syria katika eneo la mpakani la Quneitra. Hata hivyo vyombo hivyo vya habari havikutaja uwezekano wa kuwepo hasara katika hujuma hizo.

Magaidi wa Daesh wanaosaidiwa na Marekani na Israel nchini Syria

Aidha jeshi la utawala haramu wa Israel limedai kwamba, limetekeleza mashambulizi hayo ya kichokozi eti katika kujibu hatua ya kurushwa guruneti kutoka Syria kwenda katika milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Hii ni katika hali ambayo tangu mwaka 2011 kulipoibuka mgogoro wa kubuniwa na madola ya Magharibi na washirika wao katika eneo nchini Syria, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara ya mizinga au ndege zake za kivita katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ya Kiarabu. Mara zote Israel inatekeleza hujuma hizo pale magaidi wanaopata uungaji mkono kutoka Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu wanapodhoofika na kushindwa katika ulingo wa vita.

Misafara ya jeshi la Syria kuelekea walipo magaidi wa Kiwahabi washirika wa Israel

Kupitia hujuma hizo, Israel huwa inalenga misafara ya silaha na zana za kijeshi ya serikali ya Damascus kwa ajili ya kuwaangamiza magaidi ambapo baada ya hapo huwa inawaokoa magaidi hao. Jeshi la Syria limetangaza mara kadhaa kwamba, kila mara magaidi hao wanapozidiwa, Israel huwa inashambulia askari wa serikali kwa kisingizio hicho cha kurushwa kombora kutoka ardhi ya Syria kwenda ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Tags

Oct 20, 2017 04:40 UTC
Maoni