• Hizbullah: Saudia imeshindwa kuunda muungano wa kukabiliana na sisi

Mjumbe wa Baraza Kuu la harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, matukio mapya katika eneo la Mashariki ya Kati yanajiri kwa maslahi ya muqawama, kama ambavyo yanapingana na mtazamo wa Marekani, Israel na Saudi Arabia.

Sheikh Nabil Qaouk amefafanua kuwa, Harakati ya Hizbullah inapambana katika maeneo tofauti ya Syria kwa ajili ya kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh kwa kuwa usalama na amani ya Lebanon unategemea kuangamizwa makundi ya kigaidi ya Daesh na Jab'hatu Nusra.

Mfalme wa Saudia

Mjumbe wa Baraza Kuu la harakati ya Hizbullah ameongeza kuwa, miaka miwili iliyopita Saudia na ikishirikiana na utawala haramu wa Israel iliiwekea vikwazo harakati hiyo kwa kuliweka jina lake katika orodha ya makundi ya kigaidi. Amesema kuwa hadi sasa njama hizo za Saudia na washirika wake zimefeli vibaya. 

Sheikh Nabil Qaouk amesisitiza kuwa, hasira za Saudia na Marekani ni ishara ya kukosa matumaini na kudhoofika kwao kuzuia uwezo wa muqawama. Kadhalika kiongozi huyo wa Hizbullah Lebanon ameongeza kuwa, kwa kutumia fedha, Riyadh inatekeleza njama kuishinikiza Lebanon ili isimame dhidi ya harakati hiyo na kwamba njama hizo pia zimeangukia pua.

Magaidi wakufurishaji wa Kiwahabi wanaofanya jinai nchini Syria kwa fedha za Saudia

Itakumbukwa kuwa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon imekuwa mstari wa mbele katika kuzuia njama za madola yenye kupenda kujitanua katika eneo la Mashariki ya Kati yaani Marekani, Israel, Saudia na kadhalika za kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria kupitia makundi ya kigaidi na ya kiwahabi yanayopata misaada ya kila upande kutoka kwa madola hayo.

Tags

Oct 22, 2017 03:06 UTC
Maoni