• Indhari ya rais wa Afghanistan kwa nchi zinazounga mkono ugaidi

Rais Mohammad Ashraf Ghani Ahmadzai wa Afghanistan amezionya nchi zinazounga mkono wimbi la ugaidi katika eneo.

Sambamba na Rais Ashraf Ghani kutoa indhari hiyo ametangaza kuwa, nchi zinazoyaunga mkono magenge ya kigaidi nchini Afghanistan zitaanza kutengwa hatua kwa hatua. Aidha rais huyo amelaani mashambulizi ya hivi karibuni nchini humo ambayo yamesababisha makumi ya watu kuuawa. Itakumbukwa kuwa siku ya Alkhamis, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Taleban lilishambulia kambi moja ya jeshi la serikali katika mkoa wa Kandahar, shambulizi lililosababisha makumi ya askari kuuawa. Aidha Waislamu zaidi ya 72 wakiwemo wanawake na watoto waliuawa siku ya Ijumaa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga misikiti miwili ya Waislamu wa Suni na Shia katika miji ya Kabul na Ghor nchini Afghanistan.

Wanachama wa kundi la kigaidi na Kiwahabi la Taleban nchini Afghanistan

Baada ya mashambulizi hayo, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) lilijigamba na kutangaza kuwa ndilo lililohusika na jinai hizo. Wiki hii makundi ya Taleban na Daesh yamefanya mashambulizi mengi ya kigaidi katika miji tofauti ya Afghanistan na kusababisha watu wengi kuuawa na kujeruhiwa. Hii si mara ya kwanza kwa Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan kuzinyooshea kidole cha lawama nchi zinazoungaji mkono ugaidi. Kwa miaka mitatu sasa Rais Ghani amekuwa akizionya baadhi ya nchi za eneo juu ya mwenendo wao katika kuunga mkono makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kuchupa mipaka. Kabul inaituhumu Pakistan kuwa muhusika mkuu wa vitendo vya ukatili na mauaji sambamba na kuchochea vita nchini Afghanistan.

Miripuko ya kigaidi inayoteketeza maisha ya raia wa Afghanistan wasio na hatia

Atiqullah Amarkhel, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Afghanistan anasema: "Magaidi wanaotenda jinai nchini humo, wanapata uungaji mkono kutoka Pakistan na ikiwa Islamabad itasitisha mwenendo wake huo, basi magaidi hao hawatakuwa na uwezo tena wa kukabiliana na jeshi la serikali ya Afghanistan." Mwisho wa kunukuu. Matamshi mapya ya Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan kuzielekea nchi zinazounga mkono ugaidi nchini kwake, yanahusiana moja kwa moja na ongezeko la mashambulizi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ndani ya siku za hivi karibuni. Hasa kwa kuzingatia kuwa mashambulizi ya Daesh siku ya Ijumaa mjini Kabul na Ghor yameua kidhulma Waislamu 90 wasio na hatia. Aidha shambulizi jingine la Jumamosi ya jana lililofanywa na kundi la Taleban katika chuo cha kijeshi magharibi mwa Kabul, limeua watu wasiopungua 15. Kiujumla ni kwamba, mashambulizi mtawalia katika maeneo tofauti ya nchi hiyo yanayofanywa na magenge ya Taleban na Daesh (ISIS) hata kama yanatajwa na serikali ya Kabul kuwa yanachochewa na kufadhiliwa na baadhi ya nchi zinazounga mkono magenge yenye misimamo ya kuchupa mipaka na yanayofanya uhalifu, lakini wakosoaji wa serikali wanaamini kwamba ongezeko la hujuma hizo linasababishwa na udhaifu wa serikali ya umoja wa kitaifa katika kudhamini usalama, kukabiliana na ugaidi na kuendelea kuwepo tofauti za kisiasa nchini humo kwa sasa.

Viongozi wa Afghanistan wanaotajwa kuwa na ushindani wa madaraka

Kwa mtazamo wa wapinzani hao, licha ya kuwepo uungaji mkono wa baadhi ya pande za kigeni nje ya mipaka ya Afghanistan kwa makundi ya kigaidi nchini Afghanistan,, lakini hadi sasa Rais Ghani hajawa na ratiba ya maana kwa ajili ya kukabiliana na machafuko na makundi ya kigaidi na badala yake, mivutano ya kisiasa ndani ya nchi hiyo yanaielekeza serikali ya umoja wa kitaifa kwenye njia isiyo sahihi. Hata baada ya kujiri maashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni, Mohammad Mohaqiq Makamu wa Pili wa Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan ametoa taarifa na kuwataka wanasiasa wa nchi hiyo wasianze kufanya kampeni za uchaguzi kabla ya wakati wake. na badala yake walinde umoja kati ya watu wa matabaka tofauti na halikadhalika kupambana na makundi hatari ya kigaidi yanayotishia usalama wa Afghanistan.

Oct 22, 2017 12:20 UTC
Maoni