Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex W. Tillerson jana alikuwa Riyadh huko Saudi Arabia katika awamu ya kwanza ya safari yake kwenye nchi kadhaa za Ghuba ya Uajemi.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, lengo la safari hiyo ni kufuatilia uhusiano wa pande mbili, kupunguza hitilafu zilizopo kati ya Saudi Arabia na Qatar na kuanzisha muungano mpya dhidi ya Iran.

Kwa sasa na kwa kutilia maanani kuanza kuhesabika siku za uhai wa kundi la kigaidi la Dash katika eneo la magharibi mwa Asia, Washington inafanya juu chini kuanzisha mfumo wake mpya katika eneo hilo. Miongoni mwa sifa kuu na muhimu za mfumo huo wa Kitrump katika eneo hilo ni kuiimarisha Saudi Arabia na kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni kwa sababu hiyo hiyo pia ndiyo maana katika safari yake ya kwanza nje ya nchi kama Rais wa Marekani, Donald Trump aliitembelea Saudi Arabia na kutia saini mikataba ya kijeshi na isiyo ya kijeshi yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 400. 

Muungano wa kuidhibiti Iran!!

Siasa za sasa za Marekani za kuzidisha uungaji mkono kwa Saudi Arabia katika eneo la magharibi mwa Asia zimezidisha hitilafu za miaka mingi kati ya Riyadh na Doha. Hitilafu hizo zilizidhihiri wazi zaidi baada ya Marekani na Saudi Arabia kuzidisha harakati za kuzichochea nchi za magharibi mwa Asia dhidi ya kaka mwingine mkubwa wa eneo hilo, yaani Jamhuri ya Kiislamu. Katika mtazamo wa Washington na Riyadh, kuwepo Iran inayojitawala na yenye nguvu ni kikwazo kikuu katika njia ya kuanzishwa mfumo mpya wa Kitrump katika eneo hilo. Kwa msingi huo, suala la kukabiliana na Iran kwa kutumia visingizio mbalimbali kama madai ya ukiukaji wa makubaliano ya nyuklia, kuunga mkono ugaidi na kuzitwaa ardhi za nchi nyingine, limewekwa katika ajenda ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili. Katika mchakato huu, Waisrael pia wamekuwa waitifaki wa Saudi Arabia kupitia upatanishi wa Marekani.

Pamoja na hayo yote inatupasa kuelewa kwamba, njama za sasa za serikali ya Trump za kile kinachotajwa kuwa ni kutaka kuidhibiti Iran, si jambo jipya na zilianza miongo minne iliyopita baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Karibu marais wote wa zamani wa Marekani walijaribisha bahati zao za kutaka eti kuidhibiti Iran ya Kiislamu lakini mara zote nguvu na ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati ulipanuka na kuimarika zaidi. Nafasi maalumu ya kijiografia ya Iran, jamii hai na yenye utanashati, miundombinu ya viwanda na ruwaza njema za masuala ya kiroho na kimaadili vimeipatia Iran nafasi makhsusi na uzito mkubwa licha ya njama na hila zote zinazofanywa na maadui kila uchao.

Trump akidansi na Mfalme wa Saudia

Kwa sasa Marekani na washirika wake wa kikanda kama Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel zinalenga shabaha uwezo na ushawishi wa jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah). Katika wiki za hivi karibuni maafisa wa serikali ya Marekani walisema kinagaubaga kwamba, wanataka kupunguza ushawishi na mchango wa jeshi hilo la Sepah nje ya mipaka ya Iran kupitia njia ya kuliwekea vikwazo na kutenganisha baina ya Iran na marafiki zake hususan Iraq. Ni kwa msingi huo ndiyo maana mashauriano juu ya jinsi ya kuliwekea vikwazo jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na kufanya upatanishi kati ya Baghdad na Riyadh vikapewa kipaumbele katika harakati za kisiasa za Tellarson kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi.

Pamoja na hayo yote, historia, ada, mila, utamaduni wa eneo hilo, rundo kubwa la hitilafu, ushindani na uhasama uliopo baina ya nchi za Kiarabu vimezuia na vitaendelea kuzuia kuundika muungano dhidi ya Iran kwa mujibu wa matakwa ya Wamarekani.     

Oct 23, 2017 09:00 UTC
Maoni