• Jeshi la Lebanon lawekwa katika hali ya tahadhari kutokana na chokochoko za Israel

Mkuu wa Jeshi la Lebanon amewataka wanajeshi wa nchi hiyo kuwa katika hali ya tahadhari hususan katika maeneo ya mpaka wa kusini, ili kuzima chokochoko zozote zinazoweza kuanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jenerali Joseph Aoun amewataka wanajeshi wa nchi hiyo kuwa macho na kutekeleza Azimio Nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kulindwa uthabiti katika mpaka wa nchi hiyo na ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. 

Aoun ameandika katika ukurasa wake mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Nakutakeni muwe macho na kuwa tayari kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote utakaoanzishwa na adui Israel katika mpaka wetu wa kusini. Ishara zote zinaonyesha kuwa kuna njama za kuvamiwa Lebanon, raia wake na jeshi lake."

Israel inapanga kuishambulia tena Lebanon kwa nikaba ya Saudia

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alifichua kuwa, Saudi Arabia imeiomba Israel ianzishe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na Hizbullah na kwamba utawala wa Aal Saud uko tayari kutumia mabilioni ya dola kufikia lengo hilo.

Sayyid Nasrullah alisema Saudia inaogopa kukabiliana ana kwa ana kijeshi na Iran hivyo inataka kulipiza kisasi cha kushindwa kwake huko kupitia kuishambulia Hizbullah.

Baada ya Riyadh kumshinikiza Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri ajiuzulu akiwa Saudi Arabia, iliwataka raia wake waanze kuondoka Lebanon haraka iwezekanavyo.

Tags

Nov 22, 2017 03:04 UTC
Maoni