• Hariri arejea Lebanon, ombi lake la kujiuzulu lasimamishwa, akutana na Rais Aoun

Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon amesimamisha kwa muda ombi lake la kutaka kujiuzulu wadhifa wake huo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Michel Aoun mjini Beirut.

Hariri alirejea nchini Lebanon usiku wa kuamkia jana baada ya kuwa kwa muda nchini Saudi Arabia na kuzitembelea Ufaransa, Cyprus na Misri.

Hapo jana Hariri pamoja na Rais Michel Aoun na Spika wa Bunge Nabih Berri walihudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 74 ya uhuru wa taifa hilo kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Baada ya hapo alisema: "Nimekabidhi barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Michel Aoun lakini amenitaka nusibiri tufanye mazungumzo zaidi na nikakubali ombi lake." 

Rais Michel Aoun wa Lebanon (Kushoto) na Saad Hariri

Saad Hariri alitangaza kujiuzulu ghafla nafasi ya Waziri Mkuu wa Lebanon tarehe Nne mwezi huu wa Novemba kupitia ujumbe alioutuma kwa njia ya video kutokea nchini Saudia.

Akiwa nchini Saudia, viongozi wa Lebanon walitangaza kwamba, Hariri alikuwa anashikiliwa nchini humo na kwamba hata kujiuzulu kwake kulitokana na mashinikizo ya watawala wa Aal-Saud.

Tags

Nov 23, 2017 03:26 UTC
Maoni