• Mgogoro baina ya Qatar na nchi za Kiarabu umezidi kupamba moto

Kwa mara nyingine tena nchi za Saudia, Imarati, Misri na Bahrain zimetoa tuhuma kali dhidi ya Qatar kwa kudai kuwa inaunga mkono ugaidi. Jana usiku nchi hizo ziliongeza katika orodha yao ya makundi ya kigaidi taasisi mbili na watu 11 ambao zinadai wanafanya ugaidi kwa uungaji mkono wa Qatar.

Taasisi hizo ambazo Saudi Arabia na wenzake wameziingiza kwenye orodha yao ya makundi ya kigaidi ni Umoja wa Kimataifa wa Maulamaa wa Kiislamu na Baraza la Kimataifa la Kiislamu kwa madai kuwa taasisi hizo zinatumia vibaya Uislamu kama pazia la kuchochea vitendo vya kigaidi.

Nchi hizo zimedai kuwa watu 11 walioingizwa katika orodha ya makundi ya kigaidi wanapokea misaada kutoka Qatar kwa ajili ya kuendesha operesheni za kigaidi katika maeneo tofauti duniani.

Mzozo baina ya Saudia na Qatar

 

Saudia, Misri, Imarati na Bahrain zinaituhumu Qatar kuwa inawaunga mkono, inawapa kimbilio na misaada ya kifedha magaidi pamoja na kuchochea misimamo mikali na ya chuki.

Tarehe 5 Juni mwaka huu, nchi hizo nne zinazoongozwa na Saudi Arabia zilikata uhusiano wao wote na Qatar na kufunga mipaka yao yote ya ardhini, baharini na angani.

Tarehe 23 Juni nchi hizo nne za Kiarabu zilitoa orodha ya mambo 13 kama masharti ya kurejesha uhusiano wa kawaida na Qatar, masharti ambayo yamekataliwa kikamilifu na Doha. 

Miongoni mwa masharti hayo 13 ni kuitaka Qatar ikate uhusiano wa kidiplomasia na Iran na isiwe na uhusiano na harakati za Kiislamu zinazopambana na utawala wa Kizayuni wa Israel kama vile Hamas ya Palestina na Hizbullah ya Lebanon.

Tags

Nov 23, 2017 07:19 UTC
Maoni