Bila ya kujali utukufu wa eneo alipozaliwa Nabii Isa AS, kwa mara nyingine jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeuvamia mji wa Baytullahm (Bethlehem) na kuwashambulia kwa mabomu ya kutoa machozi Wapalestina waliokuwa wanaandamana kupinga siasa za kiuadui za Marekani dhidi ya eneo hilo takatifu.

Wakiwa wamebeba bendera za Palestina, baadhi ya waandamanaji walikuwa wamevaa nguo za Santa Claus kuadhimisha X-Mass na mwaka mpya wa Milaadia.

Hata hivyo katika kuonesha kuwa hawajali matukufu ya dini yoyote ile, wanajeshi wa Kizayuni wamewashambulia Wapalestina hao kwa mabomu ya kutoa machozi na kuwasababishia matatizo ya kupumua. 

Mkazi mmoja wa mji wa Baytullahm (Bethlehem), Mohammad al Lahhm amesema wakati Santa anatuma ujumbe kwa watoto wa Palestina kwamba "tuko katika njia ya ukombozi kuelekea Quds, na wakati Papa Noel akiwa (Santa Claus) anagawa zawadi, wavamizi wa Quds (Israel) wao wanagawa mabomu. Haya mabomu tunayopigwa na Israel leo ndiyo zawaidi yao ya X-Mass kwetu."

Viongozi mbalimbali wa Kikristo huko Palestina wamesimama imara kukabiliana na Wazayuni na kupinga kitendo cha rais wa Marekani, Donald Trump cha kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti mji mkuu wa Israel.

Miongoni mwa upinzani uliooneshwa na makundi kwa makundi ya Wakristo hao ni kuvunja ziara zao walizopanga kuzifanya katika mji alipozaliwa Nabii Isa AS wakati huu wa X-Mass baada ya Marekani kuitaja Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Hayo ni kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa Quds (Jerusalem), Pierbattista Pizzaballa. 

Itakumbukwa kuwa, siku ya Alkhamisi, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipuuza vitisho vya Marekani na kupitisha kwa kura mutlaki muswada wa kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa Palestina na si Israel.

Tags

Dec 24, 2017 16:41 UTC
Maoni