Jan 02, 2018 04:14 UTC
  • Saudi Arabia na Imarati zafadhili njama ya mapinduzi dhidi ya Mfalme wa Jordan

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimefichua njama iliyopangwa na wanawafalme watatu wa Jordan kwa ajili ya kumpindua Mfalme wa nchi hiyo kwa kusaidiwa na Saudi Arabia na Imarati.

Gazeti la Kizayuni la Israel Times limezinukuu baadhi ya duru na kuandika kuwa, vyombo vya kiintelijensia vimenasa mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa kati ya makaka wawili na mwana wa kiume wa ami yake Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan na maafisa wa Saudia na Imarati kwa ajili ya kumuondoa madarakani mfalme wa Jordan. 

Mfalme wa Jordan hivi karibuni alitoa dikrii na kuwafuta kazi jeshini wanawafalme hao kwa majina ya Faisal na Ali bin al Hussein  ambao ni ndugu zake na pia Talal bin Mahmoud mwana wa ami yake ili kuzuia mapinduzi dhidi ya utawala wake na hivi sasa wanawafalme hao watatu wanaishi chini ya udhibiti wa vyombo vya usalama. 

Tovuti ya habari ya Britt Bart News ya Marekani pia imeandika kuwa: Wanawafalme hao watatu walikuwa wakipanga njama ya kumpindua Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan kwa kushirikiana na makamanda wa Saudi Arabia. 

Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia alijaribu kumzuia Mfalme Abdallah kushiriki kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) kuhusu Quds ambacho kilifanyika hivi karibuni katika mji wa Istanbul Uturuki. Hata hivyo Mfalme wa Jordan alihudhuria kikao hicho kinyume na matakwa ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia.

Saudi Arabia ilimtuma afisa wa ngazi ya chini katika kikao hicho cha Istanbul kuhusu Quds. 

Muhammad bin Salman, Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia 

Gazeti la Kizayuni la Haaretz hivi karibuni lilitoa ripoti kuhusu uhusiano wa Jordan na Saudi Arabia na kuandika kuwa: Uhusiano wa nchi mbili hizo umekumbwa na mgogoro kufuatia siasa na hatua zinazochukuliwa na Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kwa lengo la kubadilisha muundo wa madaraka nchini humo.

Tags

Maoni