• Israel na siasa za kunyakua ardhi za Wapalestina

Kituo kimoja cha uhakiki cha Palestina kimetangaza kuwa, katika mwaka uliopita wa 2017 utawala vamizi wa Israel ulipora zaidi ya hekari 900 za ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa lengo la kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni.

Hii ni katika hali ambayo, chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel siku ya Jumapili kilipendekeza mpango wa kuunganisha vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Duru mpya ya siasa za kupenda kujitanua za utawala ghasibu wa Israel na kupendekezwa mipango ya kujitanua ya Wazayuni katika maeneo ya Palestina inafanyika kwa idhini na baraka kamili za Rais Donald Trump wa Marekani sambamba na uungaji mkono wa Washington kwa Israel katika wiki za hivi karibuni. 

Misimamo ya Donald Trump iwe ni wakati wa kinyang'anyiro cha uchaguzi nchini Marekani au baada ya hapo hasa hatua yake ya kuunga mkono ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ambao unahesabiwa kuwa wenzo wa siasa za kujitanua za Tel Aviv ni mambo ambayo kwa hakika yameupa kiburi utawala huo ghasibu cha kushadidisha siasa zake za kupenda kujitanua. Ni katika mazingira kama haya, ndio maana viongozi wa Israel wamekuwa wakitangaza bayana kwamba, siasa za kupenda kujitanua za utawala huo zinafanyika kwa uratibu na Marekani.

Avigdor Lieberman, Waziri wa Vita wa Israel

Katika uwanja huo, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel amesema kuwa, kutekelezwa mpango wa kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu hakuwezekani bila ya mwafaka wa Marekani. Avigdor Lieberman Waziri wa Vita wa Israel amesema katika mahojiano na Kanali ya Pili ya Televisheni ya Israel kwamba: Kila mtu anayedhani kwamba, anaweza kuwa na ushawishi kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan au ataweza kuendeleza ujenzi wa vitongoji hivyo bila ya mwafaka wa Marekani yuko katika makosa.

Utawala ghasibu wa Israel ukiwa na lengo la kuimarisha uwepo wake katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu ya Palestina, umekuwa ukitumia njia mbalimbali na kwa ushirikiano na uratibu na Marekani. Utawala huo ghasibu ambao ulilikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan mwaka 1967, daima umekuwa ukifanya kila uwezalo ili siku zote uwe na satuwa na udhibiti katika maeneo hayo. Siasa za kuziunganisha ardhi za Palestina na maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1967 ni miongoni mwa mipango ya Israel ya kutekeleza siasa zake za kupenda kujitanua katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ukweli ni kuwa, Israel inafuatilia kutekeleza siasa za kuunganisha ardhi za Palestina na ardhi inazozikalia kwa mabavu kwa kuanza na Beitul-Muqaddas. Israel ambayo iliyakalia kwa mabavu maeneo ya Beitul-Muuqaddas Magharibi mwaka 1948, mnamo mwaka 1967 ililidhibiti eneo la Beitul-Muqaddas Mashariki na mwaka 1981 ikaliunganisha eneo hilo na ardhi nyingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu ili kuandaa mazingira ya kulitangaza eneo hilo kuwa mji mkuu wake na kuzifanya fikra za jamii ya kimataifa zilikubali hilo.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel

Ukweli ni kuwa, Israel inataka kufuatilia pia suala hilo kwa maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa hakika Wazayuni wanataka kwa kutumia njama mbalimbali na kwa kudhibiti maeneo zaidi ya Wapalestina, kivitendo wakamilishe mwenendo wa kuyadhibiti kikamilifu maneo hayo.

Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na mkataba wa Geneva Uswisi, Israel ikiwa dola vamizi, imekatazwa kuchukua hatua yoyote ile ya kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa maeneo inayoyakalia kwa mabavu. Katika mazingira kama haya, Intifadha ya Tatu ya Wapalestina na kusimama kidete wananchi hao mkabala na utawala wa Kizayuni wa Israel inahesabiwa kuwa ngome imara na yenye taathira katika kuzuia siasa za kupenda kujitanua za utawala ghasibu wa Israel.

Tags

Jan 02, 2018 13:19 UTC
Maoni