• Utawala wa Saudia, chanzo cha mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen

Kuenea baa la njaa, maradhi na vifo vinavyotokana na mashambulio mtawalia ya Saudi Arabia na vile vile hatua ya Aal Saud ya kuizingira Yemen kumeifanya nchi hiyo masikini ya Kiarabu ikabiliwe na maafa makubwa ya kibinadamu.

Picha za kutisha na za kutia simanzi mno ambazo zimesambazwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni za kutoka nchini Yemen hususan zile zinazohusiana na watoto wa nchi hiyo ambao wameuawa kinyama kutokana na mashambulio ya mabomu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia au wale wanaopoteza maisha yao taratibu na hatua kwa hatua kutokana na lishe duni.

Baada ya kupita miezi kadhaa ya mzingiro wa kila upande dhidi ya Yemen, kumeibuka wasiwasi mkubwa wa kutokea maafa ya kibinadamu nchini Yemen. Kushadidi hali hiyo, kumeyalazimisha baadhi ya mashirika ya kimataifa kuvunja kimya chake kuhusiana na hali ya mambo nchini Yemen.

Watoto wengi nchini Yemen wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni

Matamshi ya hivi karibuni kabisa kuhusiana na suala hilo katika mwaka huu mpya ni yale yaliyotolewa na baadhi ya duru za kimataifa ambazo zimetahadharisha kuhusiana na hali ya kibinadamu nchini Yemen.  Shirika la Afya Duniani (WHO), Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa pamoja yametahadharisha kuhusiana na mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen na kusema kuwa, huo ndio mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni.

Dr Sherin Varkey, Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen amesema kuwa: Kusambaratika mfumo wa afya na tiba nchini Yemen na vile vile kuharibika mfumo wa majitaka katika nchi hiyo kumesababisha kutokea mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na maradhi mengine ya kuambukiza. 

Kabla ya hapo Mark Lowcock Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu akitoa radiamali yake kuhusiana na mzingiro wa Saudia dhidi ya Yemen alitahadharisha kwamba, kuendelea hali hiyo nchini Yemen kutapelekea kutokea ukame mkubwa katika miongo ya hivi karibuni na mamilioni ya watu watapoteza maisha yao.

Mashambulio ya Saudia yanavyoibomoa Yemen

Jamii ya kimataifa na madola makubwa duniani hayajachukua hatua yoyote ya kukabiliana na uvamizi wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ambao ndio chanzo cha maafa ya kibinadamu nchini Yemen, huku nchi kama Marekani yenyewe imekuwa ikiunga mkono kwa hali na mali jinai hizo za Saudia.

Tangu mwezi Machi mwaka 2015, Saudia, ikisaidiwa na kuungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani ilianzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Yemen kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi. Hadi sasa watu zaidi ya 13,000, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.

Upuuzaji wa Umoja wa Mataifa hususan Baraza la Usalama la umoja huo kwa mgogoro wa Yemen umekuwa ni kutoa idhini na kuupa baraka utawala wa Aal Saud ukanyage sheria na mikataba yote ya kimataifa na kushadidisha jinai zake huko Yemen. Hii ni katika hali ambayo, kushindwa Sudia kufikia malengo yake huko Yemen, kumeufanya utawala huo ukiwa na lengo la kufunika kushindwa kwake ufanye jinai kubwa zaidi. Kung'ang'ania viongozi wa Saudia suala la kuendelea na vita huko Yemen, kumeifanya hali ya kibinadamu katika nchi hiyo izidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Saudia imetupilia mbali miito inayoitaka isitishe mauaji nchini Yemen

Suala muhimu ni hili kwamba, jamii ya kimataifa kuonyesha wasiwasi na kutolewa indhari za mara kwa mara kuhusiana na mgogoro wa Yemen, kwa akali kumezifanya asasi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zilizokuwa zimenyamaza kimya, kujitokeza na kuonyesha radiamali. Katika uwanja huo, baada ya kigugumizi cha muda mrefu, hatimaye miezi kadhaa iliyopita Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia katika orodha nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto. Hii ni katika hali ambayo, takribani mwaka mmoja kabla Saudia ilikuwa imefanikiwa kushinikiza kuondolewa jina lake katika orodha hiyo baada ya kutishia kukata misaada yake kwa Umoja wa Mataifa.

Matukio ya Yemen yanaonyesha kuwa, wananchi wa nchi hiyo mbali na kukabiliwa na mashambulio mtawalia ya mabomu ya ndege za kijeshi za muungano unaoongozwa na Saudia wanakabiliwa pia na mauaji ya umati kutokana na mzingiro wa kila upande wa Saudia.

Inasikitisha kuona kwamba, jumuiya za kimataifa hazina cha kufanya ghairi ya kutoa indhari na kuonyesha wasiwasi mkubwa zilionao sambamba na kutoa misaada midogo tu isiyokuwa na maana.

Jan 03, 2018 08:09 UTC
Maoni