• Mamlaka ya Ndani ya Palestina yamjibu Trump: Quds haiuzwi

Msemaji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa jibu kwa kitisho kilichotolewa na rais wa Marekani cha kukata msaada wa fedha wa dola milioni 300 unaotolewa na nchi hiyo kwa Wapalestina kwa kusisitiza kwamba Quds si kitu cha kuuzwa kwa pesa.

Nabil Abu Rudainah amesisitiza kuwa Wapalestina hawako tayari kuanza tena kufanya mazungumzo na Israel baada ya Quds kutangazwa kuwa mji mkuu wa utawala huo wa Kizayuni na kuongeza kwamba Baitul Muqaddas ni mji mkuu wa milele wa nchi ya Palestina na wala hauuzwi kwa dhahabu au kwa mabilioni yoyote ya dola.

Wakati huohuo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema hatua ya Marekani ya kukata msaada wa fedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na pia kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina endapo haitokuwa tayari kufanya mazungumzo na mapatano na adui Mzayuni ni ghilba ya kisiasa.

Mandhari ya mji wa Baitul Muqaddas

Harakati ya Hamas imesema, uamuzi huo wa Marekani unadhihirisha uchukuaji hatua usio na tafakari wala usiojali maadili unaofanywa wa nchi hiyo na kwamba Wapalestina wanapaswa kuwa kitu kimoja na kukabiliana na mashinikizo kwa nguvu moja.

Harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina aidha imetangaza kuwa ili kukabiliana na mwenendo huo wa Marekani, nchi za Kiarabu na Kiislamu zinapaswa zitoe msaada na uungaji mkono zaidi kwa Wapalestina ili kuhakikisha wanarejeshewa haki zao.

Jana Jumanne, Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kwamba atakata misaada ya kifedha kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kutoonyesha nia ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.../

Tags

Jan 03, 2018 15:29 UTC
Maoni