Jan 12, 2018 07:48 UTC
  • Uturuki: Fitina ya kuigawa Kurdistan na Iraq, imesambaratishwa na Ankara, Tehran na Baghdad

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Süleyman Soylu amesema kuwa, fitina iliyokuwa imeratibiwa na baadhi ya madola yenye nguvu kwa ajili ya kuligawa eneo la Kurdistan na Iraq, imesambaratishwa kwa ushirikiano chanya wa Ankara, Tehran na Baghdad.

Soylu amesema kuwa, ushirikiano kati ya pande hizo umesaidia kuzima njama chafu za kuibua nchi nyingine ambayo ingekuwa kibaraka katika eneo hilo. Kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo hilo la Kurdistan ambayo ilikabiliwa na upinzani mkali wa dunia pamoja na serikali ya Iraq, ilifanyika tarehe 25 Septemba mwaka jana, kwa ung'ang'anizi wa Masoud Barzani, aliyekuwa rais wa eneo hilo.

Masoud Barzani aliyekuwa kiongozi wa Kurdistan

Hatua hiyo ilikuwa ukiukaji wa wazi wa katiba ya Iraq. Baada ya kura hiyo ya maoni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki na serikali kuu ya Iraq zilichukua hatua kali za pamoja ikiwa ni pamoja na kufunga mipaka yao na eneo la Kurdistan, suala ambalo lililifanya eneo hilo kurudi nyuma na kutupilia mbali matokeo ya kura hiyo. Wiki moja baada ya hatua hiyo, jeshi la Iraq lilianza kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyokuwa dhidi ya eneo la Kurdistan, huku serikali ya eneo hilo sambamba na kukubali kusimamisha matokeo ya kura hiyo, ikitaka pia kufanya mazungumzo na serikali ya Baghdad kwa mujibu wa katiba ya Iraq. Vilevile Masoud Barzani alilazimika kujiuzulu wadhifa wake.

Süleyman Soylu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki

Kuzimwa njama ya kutaka kuligawa taifa la Iraq, kulitafsiriwa kuwa ni pigo kubwa dhidi ya Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo daima zilikuwa zikiwachochea viongozi wa Kurdistan kujitenga na Iraq. Itakumbukwa kuwa, baada ya kufeli njama chafu kupitia genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini Iraq na Syria, pande tatu hizo zilikusudia kuigawa Iraq, suala ambalo limefeli.

Tags

Maoni