• Wapinzani Saudia waunda harakati mpya, serikali nayo yatwaa kampuni ya Bin Laden

Wapinzani wa utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia wanajiandaa kutangaza harakati mpya kwa jina la 'Al-Karamah' ambayo itapigania marekebisho muhimu ya kisiasa na kutetea harakati za mapambano ya ukombozi huko Palestina na Lebanon.

Mtandao wa Habari wa al-Ahd umeandika kuwa, kiongozi wa harakati hiyo ni Maan bin Ali al-Dowaish al-Jarba na kwamba itajikita katika kupigania marekebisho na kuwatetea raia wa Saudia ambao kwa muda sasa wamekuwa wakikandamizwa na utawala wa kifalme wa Aal-Saud.

Watawala wa sasa wa Saudia na ambao wanakosolewa kila upande kwa kujipendekeza kwa US na Israel

Kadhalika harakati hiyo ya al-Karamah imetangaza uungaji mkono wake kwa harakati za muqawama za Palestina na Lebanon ambazo zinapambana na utawala haramu wa Israel.

Hayo yanajiri katika hali ambayo duru za ndani nchini Saudia zimetangaza kwamba viongozi wa utawala wa nchi hiyo wanakusudia kuzitwaa kwa nguvu baadhi ya milki za kampuni ya 'Bin Laden Holding' na hadi sasa uongozi wa kampuni hiyo umechukuliwa na serikali na kwamba Riyadh imekusudia kutwaa pia mali na fedha zake.

Kampuni ya ujenzi ya Bin Laden, Saudia

Kampuni ya Bin Laden Holding ambayo linafahamika kuwa shirika kubwa la ujenzi duniani iliasisiwa mwaka 1931 na Muhammad Ibn Laden, baba yake Osama Bin Laden, kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Qaidah. Kutokana na mahusiano mazuri yaliyokuwepo kati ya Muhammad Bin Laden na Mfalme Abdulaziz Aal-Saud, mwasisi wa utawala wa Saudia, kampuni hiyo ilitiliana saini na serikali kwa ajili ya kuendesha harakati zake nchini humo.

Jan 12, 2018 07:54 UTC
Maoni