• Hariri aipongeza Hizbullah, ataka uhusiano uliobora na Iran

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri ametoa wito wa nchi hiyo kuwekwa mbali na migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati huku akiipongeza Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini hiyo kwa jitihada zake za kupunguza taharuki katika eneo.

Katika mahojiano na jarida la The Wall Street Journal, Hariri amesema hana tatizo na Hizbullah kuendelea kuwa sehemu ya serikali ya nchi hiyo, hata baada ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu.

Amesema lengo lake ni kuhakikisha kuwa uthabiti wa kisiasa na umoja wa taifa hilo unaendelea kushuhudiwa akisisitiza kuwa serikali ya nchi hiyo ni jumuishi.

Kadhalika amesema kama tunavyomnukuu, "Hatuwezi kukubali uingiliaji wa yeyote katika siasa za Lebanon. Uhusiano wetu na Iran au Ghuba ya Uajemi unapaswa kuwa ulio bora na ambao pia una maslahi kwa taifa la Lebanon."

Hariri akisoma barua ya kujiuzulu akiwa Saudia

Itakumbukwa kuwa, Hariri akiwa chini ya mashinikizo ya watawala wa Riyadh alisoma barua ya kujiuzulu akiwa sehemu isiyojulikana nchini Saudia mnamo Novemba 4 mwaka jana, ambapo pia alitoa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti Iran na Hizbullah zinaingilia masuala ya ndani ya eneo na kwamba amejiuzulu kwa msingi huo.

Hata hivyo mapema mwezi uliopita wa Disemba Hariri alitengua rasmi uamuzi wake wa kujiuzulu na kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri la nchi hiyo.

Tags

Jan 12, 2018 13:48 UTC
Maoni