Jan 13, 2018 03:44 UTC
  • Sababu za kuongezeka mvutano kati ya Qatar na nchi nyingine nne za Kiarabu

Licha ya kupita zaidi ya miezi 7 tokea kuanza mvutano kati ya Qatar na nchi nyingine nne za Kiarabu za kundi la 3+1, si tu kwamba hakuna dalili zozote zinazoonyesha kupungua mvutano huo bali umekuwa ukiongezeka siku baada ya nyingine.

Mvutano kati ya Qatar na kundi la 3+1 ambazo ni nchi tatu wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain pamoja na Misri ulianza mwezi Juni mwaka uliopita. Uamuzi wa Qatar kutofuata siasa za kieneo za Saudi Arabia na sisitizo la serikali ya Doha la kuendelea kuwa na msimamo huru katika siasa zake za nje, ndicho chanzo kikuu cha mvutano huo ambao umepelekea Qatar kutuhumiwa kuwa inaunga mkono ugaidi. Duru mpya ya mvutano huo kati ya Qatar na nchi nne za Kiarabu zilizotajwa imekuwa ikitekelezwa kwa ajili

Mfalme Salman wa Saudia (kushoto) na Amiri Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar

ya kuishinikiza Qatar na kuonyesha kuwa ni nchi ndogo isiyoweza kufanya lolote. Akizungumzia suala hilo hapo siku ya Jumatano tarehe 10 Januari, Muhammad bin Abdurahman Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alisema kuwa hatua ya nchi nne hizo za Kiarabu ya kuiwekea vikwazo Qatar imeisababishia hasara kubwa ya kimaada na kimaanawi na kwamba vikwazo hivyo vinatekelezwa kwa ajili ya kuwadhuru watu wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Anwar Qarqash, Waziri Mshauri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati amedai kuwa ni Qatar yenyewe ndiyo imejisababishia kutengwa na kuzua mgogoro uliopo sasa. Wakati huohuo akitoa matamshi ya dharau dhidi ya Qatar, Saud al-Qahtani, Mshauri wa Idara ya Ufalme ya Saudi Arabia amesema kwamba kwa sasa hawazingatii muda uliopita tokea kuanza kutekelezwa vikwazo dhidi ya Qatar na kulitaja suala hilo kuwa dogo mno. Katika upande wa pili, ndege za kivita za Imarati tarehe 21 Disemba mwaka uliopita zilipaa katika anga ya eneo maalumu la kiuchumi la Qatar ili licha ya kuichochea nchi hiyo zijaribu kuonyesha kuwa Qatar ni nchi ndogo sana isiyoweza kufanya chochote mbele ya nchi nne hizo za Kiarabu.

Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia

Hatua hiyo ilipelekea mwakilishi wa Qatar katika Umoja wa Mataifa kuwasilisha malalamiko ya nchi yake mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo siku ya Alkhamisi tarehe 11 Januari. Sababu kuu ya kudumishwa uadui huo dhidi ya Qatar ni kuwa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi hadi sasa imethibitisha kuwa ni nchi huru isiyotaka kufuata kibubusa matakwa ya Saudi Arabia, lakini Saudia na washirika wake wameamua kuishinikiza zaidi kwa vikwazo na kujaribu kuionyesha kuwa ni nchi ndogo sana na kuwa inapasa kufuata bila masharti, matakwa ya Riyadh na washirika wake wa Kiarabu na kuwa ni kupitia njia hiyo tu ndipo inaweza kupata amani na usalama na kufikia maenedeleo inayoyataka. Sababu nyingine ni kuwa Muhammad bin Salma, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Arabia haoni tofauti yoyote kati ya siasa za ndani na nje za nchi hiyo. Kama anavyowakandamiza wapinzani wake wa ndani na kuwaweka kizuizini bila kujali, ndivyo anavyotaka kutekeleza siasa za nje za Riyadh kwa kuikandamiza nchi ndogo ya Qatar na kuilazimisha kufuata siasa za kieneo za Saudia bila masharti yoyote.

Wanawafalme wa Saudia waliotiwa nguvuni na Muhammad bin Salman

Pamoja na hayo siasa hizo za Muhammad bin Salman zimekuwa na matokeo kinyume na alivyotarajia. Kuhusiana na suala hilo, Glen Carey mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika tovuti ya Bloomberg amesema kwamba hatua ya Saudia kuiwekea vikwazo Qatar haijatatua lolote bali imezidi kuharibu uhusiano uliopo. Kuwait na Oman, wanachama wegine wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Ujaemi wameonyesha kutoridhishwa kwao na mbinu mpya ya uongozi wa Saudia. Hani Sabra, Mwanzilishi wa taasisi ya ushauri ya Alef iliyoko mjini New York Marekani pia anaamini kwamba siasa za ndani na kieneo za Muhammad bin Salman zinafanana. Licha ya kuwa siasa hizo za ukandamizaji zimemuwezesha kuwafuta wapinzani wake wa ndani walio na ushawishi mkubwa lakini zimefeli na kuzua hatari kubwa katika upeo wa kieneo. Sabra anamalizia kwa kusema kuwa kudumishwa mtazamo huo wa Muhammad bin Salman dhidi ya nchi ndogo za Kiarabu bila shaka hakutapunguza mvutano uliopo kati ya Qatar na Saudi Arabia na washirika wake bali watawala wa Saudia wanapasa kusubiri kukabiliwa na radiamali kama hiyo ya Qatar kutoka kwa nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi kama Kuwait na Oman.

Tags

Maoni