• Njama za kuvuruga muungano wa vita dhidi ya ugaidi wa Iran, Russia na Uturuki

Nchi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki zina muungano ambao si tu kuwa umeweza kufanikiwa katika medani ya vita dhidi ya ugaidi, bali pia katika mazungumzo ya kidiplomasia, muungano huo umeweza kuibua mabadiliko katika masuala yanayohusiana na tatizo la ugaidi.

Nafasi muhimu ya Iran, Russia na Uturuki katika utatuzi wa mgogoro wa ugaidi nchini Syria ni jambo ambalo limepelekea  baadhi ya madola ambayo yameshindwa na ambayo maslahi yao yamo katika kuendelea mgogoro wa Syria, yaanze kutekeleza njama za kuibua mfarakano na misuguano kati ya nchi hizo tatu.

Iran, Russia na Uturuki zimekuwa zikisimamia mazungumzo ya kuleta amani Syria ambayo ni maarufu kama Mazungumzo ya Astana na yamefanikiwa na kupata matokeo mazuri na ya haraka  ikilinganishwa na mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea bila natija yoyote huko katika miji ya Geneva na Paris.

Ushirikiano wa nchi hizo tatu ni mfano mzuri wa kuigwa wa namna ushirikiano wa kieneo unaweza kupelekea kuhitimishwa mgogoro wa ugaidi.

Pamoja na kuwepo mafanikio kama hayo, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vimekuwa vikijaribu kueneza propaganda na kukuza kupita kiasi suala la kuwepo mitazamo tafauti baina ya nchi hizi tatu. Kwa mfano vyombo vya habari vya Kimagharibi  vimekuwa vikidai kuwa, Uturuki imelalamikia nafasi ya Iran na Russia katika ukombozi wa mji wa Idlib nchini Syria na hata kudai kuwa Ankara imewaita mabalozi wa nchi hizo mbili kubainisha malalamiko yake. Habari hiyo ilikanushwa na hiyo ni ishara ya kuwepo mkakati wa kutaka kuonyesha kuna hitilafu baina ya nchi hizi tatu. Ni wazi kuwa mkakati huo wa kufarakanisha Iran, Russia na Uturuki umegonga mwamba.

Mazungumzo ya amani ya Syria katika mji wa Astana

Pamoja na hayo, kuwepo wimbi hilo la propaganda  ni nukta ambayo inapaswa kuzingatiwa na hivyo wakuu wa Iran, Russia na Uturuki wanapaswa kuchukua tahadhari ili wasitumbukie katika mtego wa baadhi ya madola ya Magharibi na Kiarabu ambayo yanasubiri kusambaratika muungano wa nchi hizi tatu na hivyo kuandaa uwanaja wa kushadidi tena mchafuko katika nchi iliyokumbwa na vita ya Syria.

Ni wazi kuwa Marekani haifurahishwi hata kidogo na nafasi ya Iran, Russia na Uturuki katika kadhia ya utatuzi wa mgogoro wa Syria. Hali kadhalika baadhi ya madola ya Kiarabu ambayo ni wafadhili wakuu wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh yanataka kuonyesha kuwa muungano wowote wa kieneo hauwezi kufanikiwa kuhitimisha migogoro ya kieneo na kwamba ni madola ya Magharibi tu na waitifaki wao ndio wenye uwezo wa eti kupambana na ugaidi.

Pengine ni kwa sababu hii ndio mwanasiasa mmoja wa Afghanistan hivi karibuni akihojiwa na vyombo vya habari vya Uingereza akajaribu kuituhumu Iran eti kuwa inaunga mkono magaidi wa ISIS nchini Afghanistan. Amedai kuwa eti lengo la Iran ni kueneza ushaiwshi wake katika mipaka yake ya mashariki na hivyo kufanya nchini Afghanistan kile ilichokifanya nchini Syria.

Tuhuma hizo zisizo na msingi na ambazo hazizingatii uhalisia wa mambo ni ishara ya hasira za Saudia na vibaraka wake katika eneo kufuatia ushindi wa Iran katika medani ya vita dhidi ya magaidi wa ISIS au Daesh. Ni kwa msingi huo ndio kukashuhudiwa uenezwaji uvumi na habari bandia dhidi ya Iran.

Magaidi wa ISIS wanaopata himaya ya baadhi ya madola ya Magharibi na Kiarabu

Kwa hivyo, mbali na nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki, madola menginezo ya Asia Magharibi na hata makundi ya wananchi kama vile Wakurdi nk, wote wanapaswa kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari kutojiingiza katika wimbi la kueneza propaganda dhidi ya mrengo unaojitahidi kurejesha uthabiti katika eneo.

Njama hizo za kuibua mifarakano zinatekelezwa na baadhi ya madola ya Magharibi na vibaraka wao katika eneo na hivyo mataifa ya eneo hayapaswi kutumbukia katika mtengo huo wa kuhasimiana na badala yake  yategemee nguvu za kieneo katika kuangamiza ugaidi.

 

Tags

Jan 13, 2018 07:39 UTC
Maoni