• Israel: Hizbullah itakuwa na uwezo wa kuvurumisha makombo 4000 kwa siku katika vita ijayo

Utawala haramu wa Israel umetangaza kupitia gazeti lake la Yedioth Ahronoth kwamba, harakati ya Hizbullah nchini Lebanon, itakuwa na uwezo wa kuvurumisha makombora 4000 kwa siku kwenda ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) katika vita yoyote ijayo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, harakati hiyo itakuwa na uwezo wa kuvurumisha makombora kuanzia 3000 hadi 4000 kwa siku, hii ikiwa na maana kwamba kwa kila saa moja itavurumisha makombora 150, suala ambalo ni hatari sana kwa Israel. Kadhalika gazeti hilo la Kizayuni limeelezea uwezo mkubwa wa makombora hayo ya Hizbullah kiasi kwamba, yanaweza kushambulia na kulenga shabaha maeneo yote ya Israel.

Mmoja wa makomando wa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon

Pia limesema kuwa, katika vita hivyo Hizbullah itatumia kwa mara ya kwanza makombora yake yenye uwezo mkubwa yakiwemo yale ya ardhi kwa ardhi kulenga shabaha. Kutokana na hali hiyo, Yedioth Ahronoth limeandika kuwa, katika vita vijavyo harakati hiyo itapanua zaidi wigo wake hadi nchini Syria. Limemnukuu Avigdor Lieberman, Waziri wa Vita wa Israel akisema kwamba kwa sasa asilimia 30 ya walowezi wa Kizayuni hususan maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, hawana maeneo ya kujificha na kuongeza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuandaa bajeti kamili kwa ajili ya kuzuia hasara zitakazosababishwa na mashambulizi ya harakati hiyo ya Kiislamu ya nchini Lebanon.

Askari wa utawala khabithi wa Israel wakilia baada ya kupata pigo kali kutoka kwa Hizbullah mwaka 2006

Pia limevielezea vita hivyo tarajiwa kuwa ni hatari ambayo itasababisha hasara kubwa katika safu ya askari wa Israel. Katika vita vya siku 33 mwaka 2006 kati ya harakati hiyo ya Hizbullah na utawala haramu wa Israel, Tel Aviv ilishindwa vibaya na kukubali kurejea nyuma.

Tags

Jan 13, 2018 14:16 UTC
Maoni