Feb 01, 2018 11:20 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Ulaya la kupatiwa suluhisho mgogoro wa Mashariki ya Kati

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema suluhisho la kuundwa nchi mbili kwa ajili ya mgogoro wa Mashariki ya Kati halina chaguo jengine mbadala la kisiasa lenye itibari na la kudumu.

Kwa mujibu wa Mogherini, msingi na lengo la taasisi hiyo ya Ulaya katika kadhia hiyo ni kupatikana suluhisho kwa njia ya kuundwa nchi mbili, huku Baitul Muqaddas ukiwa ni mji mkuu wa baadaye wa nchi hizo; uamuzi ambao msingi wake ni makubaliano ya Oslo na sheria za kimataifa yakiwemo maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Msimamo uliotangazwa na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kuhusu njia ya utatuzi wa kadhia ya Palestina unatokana na msimamo rasmi wa EU juu ya suala hilo. Na hii ni katika hali ambayo hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel, imemaanisha kivitendo kuwa Washington imeamua kulitupilia mbali suluhisho la kuundwa nchi mbili huru ndani ya ardhi ya Palestina.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya

Msimamo huo uliochukuliwa na Trump umepingwa na Umoja wa Ulaya. Kwa kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa Israel, Trump ametilia nguvu kuendelea kubaki, bali hata kupanuka zaidi mipaka ya utawala huo wa Kizayuni kwenye ardhi ulizozivamia na kuanza kuzikalia kwa mabavu mwaka 1967. Na mkabala na hilo, kwa kuzikana haki za Wapalestina kuhusiana na mji wa Quds hususan haki ya kutambuliwa kuwa mji mkuu wa nchi huru ya Palestina, Trump ameonyesha kivitendo kuwa ameachana na njia ya ufumbuzi kupitia uundaji wa nchi mbili.

Tukiachilia mbali kwamba msimamo rasmi wa Umoja wa Ulaya kuhusu kadhia ya Palestina ni kuunga mkono suluhisho la kuundwa nchi mbili ndani ya ardhi hiyo moja, lakini kiutekelezaji, umoja huo haujachukua hatua athirifu kwa ajili ya kufikiwa lengo hilo. Margaret Johansen kutoka taasisi ya utafiti wa amani na sera za kiusalama ya Chuo Kikuu cha Hamburg nchini Ujerumani anaitakidi kuwa, Umoja wa Ulaya haujachukua hatua za kutosha kwa ajili ya kuundwa nchi ya Palestina. Isitoshe, upinzani wa umoja huo kwa hatua za kivamizi na kichokozi za Israel dhidi ya Wapalestina umekuwa ni wa utoaji taarifa tu; na sana sana ni kuususia utawala huo ghasibu. 

Kwa mujibu wa Tsafrir Cohen, mkurugenzi wa Mashariki ya Karibu katika shirika la utoaji misaada ya kibinadamu la Medico International, Umoja wa Ulaya hauna nia, wala hauko katika nafasi ya kuweza kusaidia kuhitimisha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaoendelea kufanywa na Israel.

Tsafrir Cohen

Licha ya msimamo huo wa Umoja wa Ulaya kuhusu Palestina, nukta ya msingi ni kwamba kuundwa nchi mbili katika ardhi za Palestina si suluhisho linalozingatia ukweli halisi wa kadhia hiyo. Suluhisho la kuundwa nchi mbili linaikana haki ya wananchi wa Palestina ya kuwa na nchi yao huru katika ardhi yao yote ya Palestina; na badala yake linahalalisha na kuukubali rasmi uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa ardhi hiyo uliofanywa na Wazayuni kwa uungaji mkono wa Magharibi na kupelekea kuundwa utawala bandia wa Kizayuni wa Israel mwaka 1948.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa suluhisho la kiadilifu kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala la Palestina kwa kupendekeza iitishwe kura ya maoni ya kuamua mustakabali wa Palestina ambapo wakaazi wote wa asili wa Palestina wataamua kwa uhuru kuhusu mustakabali wa ardhi yao.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Katika pendekezo lake hilo, Ayatullah Khamenei amesema: "Wapalestina wote, wawe ni wale wakaazi wa sasa au wale waliohamishiwa kwenye nchi nyengine lakini wamebaki na utambulisho wao wa Upalestina, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi, washiriki kwenye kura ya maoni ya wananchi itakayofanyika chini ya usimamizi makini na wa kuaminika na kuchagua muundo wa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo; na Wapalestina wote ambao kwa miaka na miaka wamevumilia mateso ya ukimbizi warejee nchini kwao na kushiriki kwenye kura hiyo ya maoni na baadaye itungwe katiba na kuitishwa uchaguzi".../  

Tags

Maoni