Feb 08, 2018 03:58 UTC
  • Saudia yafungua rasmi anga yake kwa ajili ya ndege zinazokwenda Israel

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, Saudi Arabia imefungua anga yake kwa ajili ya ndege zinazoelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni tangu mwaka 1948 ambazo zimebadilishwa jina na kuitwa Israel.

Hayo yaliandika jana (Jumatano) na gazeti la Kizayuni la Haaretz na kuongeza kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa, Saudia imefungua anga yake kwa ajili ya safari mpya ya anga ambayo imetumiwa na ndege ya shirika la ndege la India, Air India, kuelekea Israel, suala ambalo kwa mujibu wa gazeti hilo, linaonesha namna uhusiano wa Saudia na utawala wa Kizayuni ulivyoimarika hivi sasa.

Air India limekuwa shirika la kwanza la ndege kutumia anga ya Saudi Arabia kuelekea Israel

 

Karibu mwezi mmoja uliopita, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitembelea India na kuwekeana saini na nchi hiyo mikataba mbalimbali ya uchukuzi na usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuanzishwa safari za moja kwa moja za ndege kutoka India hadi ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kabla ya hapo  shirika la ndege utawala wa Kizayuni "EL AL" lilikuwa limemtaka Netanyahu aiombe Saudia iruhusu anga yake itumiwe na ndege zitakazokuwa zinaelekea Israel kutokea India.

Itakumbukwa kuwa karibu miaka 70 sasa ndege zote zinazoelekea Israel zilikuwa zimepigwa marufuku kutumia anga ya Saudi Arabia.

Hata hivyo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudia zimeimarisha uhusiano wao na Israel na kuutangaza hadharani licha ya kwamba utawala wa Kizayuni ndiye adui nambari moja wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tags

Maoni