Feb 09, 2018 02:31 UTC
  • Onyo la Syria kuhusiana na uungaji mkono mkubwa unaofanywa na Israel kwa ugaidi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kulalamikia mashambulio mapya yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo moja lililoko kwenye viunga vya Damascus, mji mkuu wa Syria.

Siku ya Jumatano, utawala wa Kizayuni ulikishambulia kwa makombora kadhaa kituo cha utafiti wa kisayansi cha Syria kilichoko katika eneo la Jamraya kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo. Uchokozi huo wa Israel ni muendelezo wa hatua hatari na za kiadui zinazofanywa na utawala huo haramu katika eneo hili la Mashariki ya Kati, uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi, kurefusha vita na mgogoro nchini Syria na kujaribu kuyatia moyo makundi ya kigaidi yaliyoshindwa na kusambaratishwa kufuatia mafanikio makubwa liliyopata jeshi la Syria na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo.

Taswira ya hujuma na shambulio la kivamizi la Israel ndani ya ardhi ya Syria

Hatua za utawala wa kigaidi wa Israel na ushirikiano wa mtawalia unaoendelea kufanya na makundi ya kigaidi havibakishi chembe yoyote ya shaka kwamba hatari ya Israel haitafautiani na ya makundi ya kitakfiri ya Daesh na Jabhatu-Nusrah. Ukweli ni kwamba harakati za Wazayuni na magaidi ni mithili ya mbawa mbili za ndege mmoja zinazofanya kazi pamoja ya kushadidisha mauaji dhidi ya wananchi wa Syria. Kupitia ukaliaji wake wa mabavu wa ardhi ya Syria au kwa kushambulia kila baada ya muda maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan katika miaka ya karibuni, Israel imekuwa ikiendeleza kwa sura tofauti ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya ardhi yote ya Syria.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Jabhatu-Nusrah

Tangu ulipoanza mgogoro wa Syria karibu miaka saba iliyopita, utawala wa Kizayuni umefanya mashambulio ya anga mara kadhaa dhidi ya ngome za vikosi vya Syria katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kwa lengo la kuyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi yanayopigana na serikali halali ya Damascus. Syria imetanzwa na mgogoro mkubwa na mpana wa ndani kutokana na njama za Magharibi, Uzayuni wa kimataifa na vibaraka wao katika eneo. Katika kutekeleza njama hizo, utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya Magharibi yanayoipinga serikali ya Rais Bashar Al-Assad ziliyatumia vibaya malalamiko ya baadhi ya wananchi wa Syria kwa ajili ya kuyasaidia kilojistiki makundi ya kigaidi ili kuwasha moto wa machafuko ndani ya nchi hiyo. Utawala haramu wa Kizayuni, ambao una nafasi kubwa zaidi katika mgogoro wa Syria, na katika kuyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri, umevishambulia mara kadhaa vikosi vya wanamuqawama na jeshi la Syria. Ugaidi na Uzayuni ni silaha mbili zinazotumiwa na Magharibi kufanikisha malengo yake haramu katika Mashariki ya Kati. Kuhusiana na nukta hiyo, Kituo cha Daarul-Fatwa cha Palestina kimetangaza kuwa utawala wa Kizayuni na magaidi wa kitakfiri ni mithili ya pande mbili za sarafu moja.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akimjulia hali gaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh aliyepelekwa Israel kutibiwa baada ya kujeruhiwa vitani Syria 

Baada ya kubainika kuwa katika miaka ya karibuni Wazayuni wameshindwa kufanikisha malengo ya Magharibi katika Mashariki ya Kati, madola ya Magharibi yamezidisha harakati zao za kiadui kwa kuwasha moto wa ugaidi ndani ya nchi za eneo hili ili kwa kuzishugulisha nchi hizo yaweze kusaidiana na utawala wa kigaidi wa Kizayuni kufanikisha malengo yao ya kifitina na kibeberu. Katika kipindi hicho, kwa msaada wa Marekani, utawala haramu wa Israel umeutumia mtandao wa makundi ya kigaidi, ili mbali na kulitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati kwenye mgogoro na kuzidhoofisha nchi za eneo, kulifanya suala la uvamizi na ukaliaji wake wa mabavu wa ardhi ya Palestina lipuuzwe na kusahaulika.

Ni kutokana na yote hayo ndio maana tunashuhudia ushirikiano mpana na unaostawi kati ya magaidi na utawala wa Kizayuni na kushadidishwa jinai zao nchini Syria; suala ambalo limewaweka wananchi wa nchi hiyo kwenye hali ngumu. Hakuna shaka yoyote kuwa uzembeaji wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na jinai za magaidi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni ndio ulioifanya Syria iendelee kuwa uwanja wa kujifaragua utawala habithi wa Kizayuni na makundi ya kigaidi yasiyo na chembe ya ubinadamu.../

Tags

Maoni