Feb 09, 2018 06:41 UTC
  • Wapalestina na siasa za kinyama za Donald Trump

Marekani imeshurutisha suala la kuanza tena kutoa msaada kwa Wakala wa Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi wa Palesrina (UNRWA) kwa mambo ambayo yanakinzana na maslahi ya Wapalestina.

Msemaji wa UNRWA nchini Jordan, Sami Mshasha amesema serikali ya Marekani imetangaza kuwa, Washington haitatoa tena misaada kwa wakala huo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina hadi pale jumuiya hiyo itakapofanya marekebisho yanayopendekezwa na Marekani.

Duru mbalimbali za habari zimetangaza kuwa, sharti la kwanza la Marekani kwa UNRWA ni kubadilisha mada na mitaala wa masomo katika shule za Wapalestina zinazosimamiwa na wakala huo. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuondoa vipengee vyote vinavyosisitiza haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika ardhi yao iliyoghusubiwa na Israel na vilevile kufuta kipengee kinachosisitiza kuwa Quds ni mji mkuu wa serikali ya Palestina katika vitabu vya masomo. Sharti jingine la kuanza kutolewa tena misaada ya Marekani kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Palestina ni kufutwa masuala yote yanayohusiana na mapigano ya jihadi dhidi ya wavamizi na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel au Intifadha ya Wapalestina katika vitabu vyote vya shule zinazosimamiwa na UNRWA.

Watoto wa Kipalestina wakiwa shuleni

Hivi karibuni Marekani ilipunguza dola milioni 125 katika msaada wake wa kila mwaka kwa shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Palestina la UNRWA na inakusudia kupunguza dola nyingine milioni 55 katika msaada huo unaofikia dola milioni 300 kwa mwaka. Hatua hizo za kinyama za serikali ya Donald Trump dhidi ya watu wa Palestina zimekabiliwa na upinzani mkali wa taasisi na jumuiya za kiraia hata ndani ya Marekani kwenyewe. Viongozi wa jumuiya 21 za wananchi wa Marekani wametoa taarifa wakitangaza kuwa: Kukatwa misaasa ya nchi hiyo kwa UNRWA ni mwanzo hatari katika siasa za serikali ya Washington.

Maamuzi kama hayo ya Trump yanaonesha kuwa, kiongozi huyo mbaguzi hasiti kutumia njia yoyote isiyo ya kibinadamu kwa ajili ya kuwashinikiza Wapalestina na kuwazuia kudai haki zao. Ushahidi unaonesha kuwa, kuna njama mpya zinazofanywa na Marekani na Wazayuni nyuma ya pazia dhidi ya taifa la Palestina. Kwa sababu hiyo utawala haramu wa Israel umeanzisha harakati mpya za kipropaganda za kutaka kuwapokonya Wapalestina hata haki ya kuunda nchi huru ya Palestina. Sehemu moja ya njama hiyo ni mpango wa Donald Trump unaopuuza misingi yote mikuu ya malengo ya taifa la Palestina huru. Katika fremu hiyo maafisa wa serikali ya Donald Trump wanapendekeza kutafutwa nchi mbadala kwa ajili ya Wapalestina, na hapana shaka kuwa, hatua ya Trump ya kupinga katakata suala la wakimbizi wa Palestina kurejea katika nchi na ardhi yao na vilevile kuitambua rasmi Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel ni kielelezo cha njama hizo chafu.

Trump na Netanyahu

Katika uwanja huo duru mbalimbali za kisiasa zinaitambua njama hiyo mpya ya Marekani ikishirikiana na Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel kuwa ndiyo operesheni kubwa zaidi ya kutaka kufuta kabisa haki za Wapalestina kwa maslahi ya Israel. Suala hilo limezusha wasiwasi mkubwa katika duru za kimataifa.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, misaada kiduchu ya Marekani kwa wakala wa Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) si lolote si chochote ukilinganishwa na misaada lukuki ya mabilioni ya dola yanayotolewa kila mwaka na serikali ya Washington kwa utawala katili Israel unaoendelea kuua watoto wa Palestina. Hatupasi kusahau pia kwamba, Israel inaendelea kuyazingira maeneo ya Palestina kwa miaka kadhaa sasa kwa ruhusa kamili ya Marekani, mzingiro ambao unaendelea kusababisha maafa ya kutisha.

Katika mazingira kama haya inatarajiwa kuwa, jamii ya kimataifa itakomesha uzembe wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake na kuulazimisha umoja huo kuchukua hatua za maana za kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama yanayosisitiza udharura wa kurejeshwa haki za Wapalestina zilizoporwa na utawala ghasibu wa Israel.      

Tags

Maoni