Feb 09, 2018 14:09 UTC
  • Rais wa Lebanon asema jeshi la nchi hiyo liko tayari kuikabili Israel

Rais wa Lebanon ameliagiza jeshi la nchi hiyo kuwa macho dhidi ya njama zozote za utawala haramu wa Israel za kujaribu kudhalilisha uhuru wa kujitawala nchi hiyo.

Akihutubia kikao cha baraza la mawaziri hapo jana, Michel Aoun amesema nchi hiyo imejiweka katika hali ya tahadhari kujibu uvamizi na chokochoko za Israel dhidi ya ardhi au maji ya taifa hilo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Avidgor Lieberman alitoa vitisho baada ya Lebanon kutangaza zabuni za uchimbaji mafuta na gesi katika eneo la mipaka yake ya Bahari ya Mediterranean. 

Kuhusiana na kadhia hiyo, Rais wa Lebanon ameliambia baraza la mawaziri kuwa, "tunatumai mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi kwa njia za kidiplomasia, lakini nisisitize kuwa jeshi letu liko tayari kutoa jibu kali kwa chokochoko yoyote dhidi ya nchi yetu." 

Rais Aoun, Hariri na mawaziri wengine wa Lebanon

Waziri Mkuu Saad al-Hariri ambaye pia alihudhuria kikao hicho cha jana cha baraza la mawaziri amesema wameafiki kuchukua hatua kuzuia utawala haramu wa Israel kujenga ukuta baina ya Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, huku akivitaka vyama na mirengo yote ya kisiasa kuzika tofauti zao kwa shabaha ya kukabiliana kwa pamoja na uvamizi wa Israel.

Amesema maafisa wa nchi hiyo wanafanya mazungumzo na asasi za kimataifa ili kuzuia uvamizi tarajiwa wa Israel dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags

Maoni