• Israel yabomoa shule za EU huko Palestina inyaokaliwa kwa mabavu

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, Wapalestina na Mabedui wanaoishi katika kitongoji cha Area C katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina wapo katika hatari ya kufurushwa kwenye makazi yao na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Onyo hilo la UN limekuja baada ya jeshi katili la Israel kubomoa majengo ya shule mbili za chekechea zinazosimamiwa na Umoja wa Ulaya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kwa kisingizio kuwa shule hizo zimejengwa kinyume cha sheria.

Umoja wa Mataifa umesema vitendo vya namna hii vimejenga mazingira ya kuogofya kwa wanafunzi wa Kipalestina, jambo ambalo linakanyaga haki za msingi za watu wa eneo hilo, ikiwemo haki ya kupata elimu.

Watoto wa Kipalestina waliokoseshwa haki ya elimu na Israel

UN imeitaka Tel Aviv kutochukua hatua ambazo zitaendelea kuchochea idadi kubwa ya Wapalestina katika eneo hilo kukimbia makazi yao. Utawala haramu wa Israel umekuwa ukishirikiana bega kwa bega na Marekani katika kukandamiza haki za Wapalestina kila uchao. 

Hivi karibuni Marekani ilipunguza dola milioni 125 katika msaada wake wa kila mwaka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina UNRWA na inakusudia kupunguza dola nyingine milioni 55 katika msaada huo unaofikia dola milioni 300 kwa mwaka.

Tags

Feb 09, 2018 14:30 UTC
Maoni