Feb 11, 2018 07:44 UTC
  • Hizbullah: Stratijia mpya ya kupambana na uvamizi wa Israel nchini Syria imeanza rasmi

Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon imetoa taarifa ya kupongeza kitendo cha kuangamizwa ndege ya kisasa ya kivita ya utawala haramu wa Israel ya F16 katika anga ya Syria na kusisitiza kuwa, mlingano wa nguvu wa zamani sasa umebadilika.

Kanali ya televishani ya al-Manar imetoa taarifa rasmi ikiinukuuu harakati hiyo ambapo sambamba na kupongeza uwezo mkubwa wa jeshi la Syria ambao umeweza kukabiliana na hujuma za ndege za Israel na hatimaye kuiangamiza ndege hiyo muhimu ya utawala huo, imesema kuwa, hatua ya stratijia mpya kwa ajili ya kukabiliana na ukiukaji wa haki ya kujitawala wa anga na ardhi ya Syria, imeanza rasmi.

Ndege ya Israel baada ya kuangamizwa na jeshi la Syria

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: "Hizbullah inalaani vikali uungaji mkono wa wazi wa adui Mzayuni kwa makundi ya kigaidi na ya ukufurishaji na pia hatua ya Israel ya kujiingiza katika mgogoro wa Syria kupitia vitisho na uvamizi wake wa mara kwa mara. Pia tunasisitiza kwamba tukio la jana Jumamosi limemaliza kikamilifu mlingano wa zamani na kuanzisha mlingano mpya wa nguvu." Mwisho wa kunukuu.

Jeshi la Syria

Jumamosi ya jana jeshi la anga la Syria na katika kujibu mashambulizi mtawalia ya utawala wa Kizayuni ndani ya ardhi ya nchi hiyo, lilifanikiwa kuiangamiza ndege ya kivita ya Israel aina ya F16 ambapo kufuatia shambulizi hilo Israel ilipatwa na wahka mkubwa na kufanya mashambulizi mengine kadhaa ya makombora ndani ya Syria ambayo hata hivyo kikosi cha anga cha jeshi la Syria kilifanikiwa kudhibiti hujuma hizo. Wakati huo huo, Israel sambamba na kukiri kutunguliwa ndege yake hiyo ya kisasa, imeitaka Marekani na Russia kutuliza hali ya mambo na kusisitiza kwamba, haijajiandaa kuingia katika vita na Syria na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags

Maoni