• Malengo ya mazungumzo ya Kamanda wa Komandi Kuu wa Jeshi la Marekani na Amiri wa Qatar

Jumapili ya juzi ya tarehe 11 Februari, Joseph Votel, Kamanda wa Komandi Kuu ya Jeshi la Marekani alikutana mjini Doha, Qatar na Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, Amir wa nchi hiyo ya Kiarabu na kufanya naye mazungumzo.

Safari ya Kamanda wa Komandi Kuu ya Jeshi la Marekani mjini Doha imefanyika katika hali ambayo, tarehe 30 Januari mwaka huu, Marekani na Qatar zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kiistratijia ambao kwa mujibu wake Washington iliahidi kuiunga mkono Doha kutokana na uvamizi wowote ule. Safari hiyo ambayo imefanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili tu tangu kutiwa saini mkataba huo, pamoja na mambo mengine inabainisha umuhimu mkubwa ilio nao Qatar kwa Marekani.

Joseph Votel, Kamanda wa Komandi Kuu wa Jeshi la Marekani

Katika kulinda maslahi yake katika eneo la Mashariki ya Kati, Marekani kwanza inaipa uzingatiaji wa juu Qatar kutokana na nafasi yake ya kijiografia na kadhalika kutokana na utajiri wa fedha wa nchi hiyo ndogo ya Kiarabu. Inafaa kuashiria hapa kuwa, kambi kubwa zaidi ya anga ya Marekani nje ya nchi hiyo, ni kambi ya kijeshi ya Al-Udeid iliyoko nchini Qatar. Katika vita vya mwaka 2003 dhidi ya Iraq, Marekani ilitumia kambi hiyo ya anga na ambayo iko umbali wa maili 700 kutoka mji mkuu wa Iraq, Baghdad kushambulia Iraq wakati wa utawala wa Saddam Hussein. Aidha Marekani mbali na kambi hiyo ya anga ya Al-Udeid, ina kambi nyingine muhimu ya kijeshi inayofahamika kwa jina la 'as-Sayliyah' huko Qatar. Kambi ya kijeshi ya as-Sayliyah ni kambi kubwa ya Marekani ambayo ina jukumu la kuhifadhi zana za ziada za kijeshi nje ya nchi hiyo.

Joseph Votel, akiwa pia na Mohammad Bin Salman katika kuendeleza mzozo wa nchi za Kiarabu

Katika kambi hiyo kumehifadhiwa silaha mbalimbali za ziada ambapo wakati Marekani inapotaka kutuma askari zaidi katika eneo basi huwa haipatwi na wasiwasi juu ya namna ya utumaji silaha kwa ajili ya askari hao na badala yake hutumia zana za ziada zilizohifadhiwa katika kambi hiyo ya kijeshi ya as-Sayliyah. Ukweli ni kwamba, lengo kuu la kujengwa kambi hiyo ni kuharakisha shughuli ya utumaji askari zaidi wa Marekani katika eneo. Hatua ya awali ya ujenzi wa kambi hiyo ilianza mwaka 1996 huku ikikamilika mwaka 2000. Kwa kuzingatia kuwa nchi ya Qatar imekaribiana na nchi kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq, ndipo umuhimu wa nchi hiyo ukaongezeka mara dufu kwa Marekani. Mbali na jografia ya Qatar, lakini pia uchumi wa nchi hiyo ni suala ambalo linaifanya Marekani kuikodolea zaidi macho ya tamaa.

Nchi nne za Kiarabu zinazoiwekea vikwazo na mzingiro Qatar

Hii ni kusema kuwa, Qatar ni moja ya nchi tajiri zaidi za Kiarabu. Uwezo wake wa kiuchumi umeifanya iweze kuwa na kambi za kijeshi zenye kiwango cha juu na kuishawishi Marekani kwa ajili ya kuwepo kwake kijeshi ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Aidha tangu muongo wa mwaka 1990 Qatar ilianza kuwekeza zaidi ya kiasi cha zaidi ya Dola bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kambi ya Al-Udeid, kusini mwa mji wa Doha ambapo baada ya kukamilika kwake, iliikabidhi kambi hiyo kwa askari wa Marekani. Safari ya Joseph Votel, Kamanda wa Komanda wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani mjini Doha pia imefanyika kutokana na umuhimu wa kijiografia na kiuchumi wa Qatar. Serikali ya hivi sasa ya Marekani kwa upande mmoja inaitazama Qatar kutokana na umuhimu wake wa kijiografia, huku kwa upande mwingine ikifuatilia uuzaji silaha zake kwa serikali za mabepari kama vile Qatar. Malengo hayo mawili pia yanafuatiliwa na Joseph Votel katika ziara yake ya mjini Doha.

Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amir wa Qatar kulia akimcheka Mfalme Salman wa Saudia

Kuhusiana na suala hilo, Christopher M. Blanchard, mtaalamu maarufu wa nchini Marekani katika masuala ya Ghuba ya Uajemi anaamini kwamba: "Ili kudhamini kubakia na usalama na kadhalika kupunguza vitisho vya nchi  za eneo la Mashariki ya Kati zinazoizunguka nchi hiyo, Qatar inahitajia muungano wa kiusalama na Marekani kama nchi yenye uwezo mkubwa baada ya vita baridi." Mwisho wa kunukuu. Serikali ya Marekani na kwa kuzingatia mahitaji hayo ya serikali ya Doha sambamba na kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kistratijia na Qatar na kwa kisingizio cha kuidhaminia usalama, pia inaiuzia silaha zake na hivyo kuifanya Washington iweze kujidhamini mahitaji yake ya kiuchumi.

Kambi za kijeshi za Marekani nchini Qatar

Ama nukta nyingine ya kufaa kuzingatiwa ni hii kwamba, safari ya Joseph Votel nchini Qatar imefanyika katika hali ambayo hadi sasa nchi hiyo inakabiliwa na mzozo mkubwa unaoendelea kati yake na nchi nne za Kiarabu, zikiongozwa na Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri. Hata kama serikali ya Washington imekuwa na misimamo tofauti kuhusiana na mzozo huo, lakini nyaraka zinaonyesha kwamba kuendelea kwa hali hiyo ni kwa maslahi ya Washington. Hii ni kwa kuwa nchi nne zote zilizoiwekea vikwazo na mzingiro wa kila upande Qatar, ni washirika wakubwa wa Marekani kama ambavyo pia ni watekelezaji wa siasa za Washington katika eneo la Mashariki ya Kati. Ndio maana katika kuendelea mgogoro wa nchi hizo za Kiarabu Marekani haikufanya juhudi zozote za maana kwa ajili ya kuumaliza. Katika uwanja huo akiwa mjini Doha Kamanda wa Kamandi Kuu wa Jeshi la Marekani ameitaka Qatar kujizuia dhidi ya nchi nne zinazoiwekea vikwazo na mzingiro.

Feb 13, 2018 07:36 UTC
Maoni