• Kiongozi wa DAESH Abu Bakr al-Baghdadi angali hai nchini Syria lakini amejeruhiwa vibaya

Mkuu wa Idara ya Intelijinsia na Kukabiliana na Ugaidi ya Iraq amesema, kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) Abubakar al-Baghdadi angali hai na anapatiwa matibabu katika kituo kimoja cha tiba kaskazini mashariki mwa Syria baada ya kujeruhiwa vibaya katika shambulio la anga.

Abu Ali al-Basri, amenukuliwa na gazeti rasmi la serikali la nchi hiyo la Al-Sabah akieleza kuwa wana taarifa zisizoweza kukanushika na nyaraka kutoka duru za ndani ya kundi hilo la kigaidi zinazothibitisha kuwa al-Baghdadi angali hai lakini anaendelea kujificha kwa msaada wa wasaidizi wake.

Amefafanua kuwa, kiongozi huyo wa Daesh hivi sasa yuko kwenye eneo la jangwa la Jazeera magharibi mwa mkoa wa Deir Az Zor nchini Syria.

Al Basri ameongeza kuwa A-Baghdadi anasumbuliwa na majeraha, ugonjwa wa kisukari na mivunjiko ya mwili na miguu inayomfanya ashindwe kutembea bila ya kusaidiwa.

Hata hivyo haijaeleweka ni mashambulio ya anga ya nchi au upande gani yaliyosababisha kujeruhiwa kiongozi huyo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Magaidi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIL) 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Intelijinsia na Kukabiliana na Ugaidi ya Iraq Al- Baghdadi alijeruhiwa katika mashambulio ya anga yaliyofanywa ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Hapo awali Wizara ya Ulinzi ya Russia iliwahi kutangaza kuwa huenda ikawa imemuua Al-Baghdadi katika moja ya mashambulio iliyofanya kwenye viunga vya mji wa Raqqa nchini Syria.

Kanali ya televisheni ya CNN iliwanukuu maafisa wa Marekani hapo jana wakieleza kuwa kiongozi huyo wa Daesh (ISIS) alijeruhiwa huko Raqqa na kumfanya ashindwe kuongoza harakati za kijeshi za kundi lake kutokana na majeraha aliyopata.../ 

Tags

Feb 13, 2018 16:44 UTC
Maoni