• Palestina; kadhia ya kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu

Kikao cha mashauriano cha Mkutano wa Kimataifa wa Wapenzi wa Ahlul-Beit (as) kilimalizika juzi Jumatatu hapa mjini Tehran na kusisitiza juu ya udharura wa kuipa umuhimu maalumu kadhia ya Palestina ikiwa kama ndio suala na daghadagha ya kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Kikao hicho kilifanyika kwa kuhudhuriwa na makumi ya shakhsia kutoka maeneo mbalimbali ya Ulimwengu wa Kiislamu. Washiriki wa kikao hicho wametoa taarifa inayotaka kuweko uratibu mpya na hatua za kisiasa, kihabari, kiutamaduni na kivitendo kwa shabaha ya kuukomboa mji wa Beitul-Muqaddas. Aidha taarifa hiyo imesisitiza juu ya uudharura wa kuimarishwa muqawama na mapambano ya Kiislamu na vita dhidi ya makundi ya kitakfiri na kigaidi. 

Kadhia ya Palestina ilianza ghafla baada ya kukabiliwa kwa mabavu sehemu ya ardhi yake na ikaingia katika marhala na hatua tata zaidi kwa kufukuzwa na kubaidishwa mamilioni ya wananchi wa Palestina kutoka katika ardhi zao.

Msikiti wa al-Aqswa

Hivi sasa njama hizo zimeingia katika hatua nyingine baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuutangaza mji wa Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Saadullah Zarii mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati anasema:

"...Kile ambacho tunakishuhudia hii leo katika uga wa kimataifa ni kuharakisha Marekani na vibaraka wake kulifunga faili la Palestina kwa mujibu wa matakwa ya utawala ghasibu wa Israel katika hali ambayo, ushindi mtawalia wa kambi ya muqawama umeweza kuondoa sehemu muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu kutoka katika satwa ya Marekani, Israel na vibaraka wake."

Hii leo njama za Marekani na utawala vamizi wa Israel zinalilenga eneo lote la Mashariki ya Kati na ardhi za Waislamu. Hapana shaka kuwa, katika kipindi hiki nyeti, UIimwengu wa Kiislamu una majukumu mazito na makubwa zaidi na hivyo haipasi kuruhusu malengo matukufu ya Palestina yawekwe kando.

Imam Ruhullah Khomeini MA muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Imam Ruhullah Khomeini MA muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho kila mwaka ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds na hivyo kuiunga mkono Palestina, hatua ambayo iliingiza Palestina katika uga wa kimataifa na kwa mtazamo na fikra hiyo, akaonyesha kwamba, suala la Palestina ni kadhia ya kwanza na kuu katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika miaka yote hii, Marekani na utawala ghasibu wa Israel zimekuwa zikifuatilia kuisambaratisha kadhia ya Palestina na kudhoofisha muqawama na wakati huo huo kuzishughulisha nchi za Kiislamu na changamoto za ndani pamoja na mizozo bandia.

Hata hivyo hivi sasa mahesabu katika eneo hili la Mashariki ya Kati yamo katika hali ya kubadilika. Abdel Bari Atwan, mchambuuzi mtajika katika ulimwengu wa Kiarabu ameashiria katika makala  yake katika gazeti la Rai al-Yaoum juu ya kutunguliwa ndege vamizi ya kijeshi ya Israel katika anga ya Syria na kuitaja siku hiyo kuwa ya kihistoria.

Ayatullah Ali khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kwa hakika kadhia ya Palestina na Quds ni mlolongo wa njama kubwa za Uzayuni ambazo haziwezi kufikia tamati kwa kutiwa saini mikataba eti ya mapatano; bali njia pekee ya utatuzi wa jambo hilo ni kuimarishwa harakati za muqawama wa Kiislamu na kusimama kidete mbele ya utawala vamizi wa Israel.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema alipokutana na wageni walioshiriki mkutano wa 13 wa Mabunge ya Kiislamu kwamba, kuitetea Palestina ni jjukumu la wote na akasisitiza kuwa, haipaswi kudhani kwamba, kukabiliana na Israel ni jambo lisilo na faida bali kwa tawfiki na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, mapambano dhidi ya Israel iko siku yatazaa matunda kama ambavyo mapambano hayo hivi sasa yamepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.

Feb 14, 2018 02:50 UTC
Maoni