• Nujaba ya Iraq yasema itapambana na Israel ikiiletea chokochoko Hizbullah

Harakati ya Nujaba ya Iraq imesema itaiunga mkono kikamilifu harakati ya Hizbullah ya Lebanon iwapo italazimishwa kuingia katika vita vipya na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akram al-Kaabi, Katibu Mkuu wa Harakatu al-Nujaba ya Iraq aliyasema hayo jana akiwa safarini mjini Beirut na kuongeza kuwa: "Harakati yetu nchini Iraq itasimama na Hizbullah katika shambulizi lolote la Israel dhidi harakati hiyo ya Lebanon. Nujaba itasimama kwenye safu moja na Hizbullah dhidi ya chokochoko za Israel, kama tulivyosimama na harakati hiyo katika mapambano yake dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq."

Amesisitiza kuwa, muungano wa harakati mbili hizo za mapambano ya Kiislamu ya Lebanon na Iraq utazidi kushirikiana na kufanya kazi bega kwa bega katika siku za usoni. 

Wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah alifichua kuwa, Saudi Arabia imeiomba Israel ianzishe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na Hizbullah, na kwamba watu wa Saudia wako tayari kutumia mabilioni ya dola kufikia lengo hilo.

Jeshi la Israel lilishindwa vibaya na kupata hasara kubwa katika vita dhidi ya Hizbullah, kwenye msimu wa joto kali mwaka 2006. 

Tags

Feb 14, 2018 07:33 UTC
Maoni