• Sisistizo la Iran la kushiriki katika kuijenga Iraq katika kipindi cha baada ya Daesh

Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameelekea nchini Kuwait kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Kuijenga Upya Iraq. Katika safari hiyo Zarif anaongoza ujumbe wa kisiasa na kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wawakilishi wa nchi zaidi ya 70 duniani na mashirika ya uwekezaji karibu elfu mbili kutoka nchi mbalimbali wanahudhuria pia Mkutano huo wa Kimataifa wa Kuijenga Upya Iraq huko Kuwait. Kabla ya mkutano huu, Iran ilikuwa tayari imesaidia pia katika ujenzi mpya wa Iraq. Aidha miaka kadhaa iliyopita Iran ilishiriki katika kuijenga upya Iraq katika nyanja mbalimbali kama kuimarisha huduma za umeme na nishati na kuyafanyia ukarabati wa maeneo matakatifu ya kidini. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilevile ilikuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na kukombolewa maeneo yaliyokuwa yanashikiliwa na kundi hilo. Zaidi ya hayo, kuongezeka nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na masuala ya kiusalama yanayolihusu eneo hili kumeandaa mazingira mazuri ya kushirikiana kati ya nchi mbili hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa serikali na wananchi wa Iraq katika vita dhidi ya Daesh na makundi mengine ya kitakfiri nchini humo na vilevile katika kuijenga upya Iraq na kusema kuwa: Iran imetimiza majukumu na ahadi ilizotoa katika mkutano uliopita wa kuijenga upya Iraq na katika marhala hii pia imejiandaa kwa nguvu na uwezo wake wote kushiriki katika mchakato wa ujenzi mpya na ustawi wa Iraq; na hivyo kuwa bega kwa bega na serikali na wananchi wa nchi hiyo.  

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Ujenzi na ukarabati wa maeenro yaliyoharibiwa baada ya vita ni mchakato wenye nafasi muhimu katika kuzuia kuibuka tena migogoro. Wakati huo huo ujenzi huo mpya unaweza kutathminiwa katika fremu ya maslahi ya kiutamaduni na ya yale ya pamoja ya kidini. Kushiriki katika ujenzi mpya wa Iraq baada ya Daesh pia kunafanyika katika fremu hiyo hiyo. 

Kiujumla tunaweza kusema kuwa harakati hiyo ya kimataifa ina umuhimu katika pande mbili. Katika upande wa kwanza, ni kuisaidia Iraq katika ujenzi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa nchi hiyo sambamba na kukarabati miundo mbinu iliyoharibiwa huku upande wa pili ukiwa ni umuhimu kuimarisha hali ya utulivu na usalama huko Iraq na katika kanda nzima kwa ujumla.  

Kwa vyovyote vile hatua ya kuijenga upya Iraq ni fursa kwa ajili ya kufidia sehemu ya maafa na uharibifu mkubwa uliosababishwa na kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq japokuwa baadhi ya uharibifu uliofanywa na Daesh huko Iraq hauwezi kufidiwa kama vile athari za kale za kiutamaduni zilizoharibiwa katika mji wa Nimrud nchini humo.

Magaidi wa Daesh wakibomoa athari za kale katika mji wa Nimrud Iraq 
 

Hata hivyo hatupasi kusahau kuwa, sehemu ya uharibifu mkubwa huko Iraq ni matokeo ya hatua za waungaji mkono wa magaidi katika kalibu ya muungano wa kimataifa eti wa mapambano dhidi ya ugaidi chini ya uongozi wa Marekani. Tathmini mpya zinaonyesha kuwa, kiwango cha hasara na maafa yaliyosababishwa na muungano huo wa kijeshi kwa miundo mbinu ya Iraq ni cha dola bilioni 45. 

Gazeti la Wall Street Journal limeandika: Katika tathmini mpya iliyofanywa na Benki ya Dunia na serikali ya Baghdad imebainika kuwa, muungano wa kimataifa eti wa kupambana na ugaidi unaoongozwa na Marekani umesababisha maafa makubwa kwa miundo mbinu ya Iraq zikiwemo shule, vituo vya nishati, nyumba za raia na miundo mbinu mingine ya kiraia nchini humo. 

Feb 14, 2018 08:21 UTC
Maoni