• Guterres: Kuijenga upya Iraq kunahitajia umoja wa kitaifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono ubunifu wa kila namna uliotolewa kuhusu kuijenga upya Iraq na kusisitiza kuwa, ujenzi mpya wa nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita unahitajia umoja wa kitaifa kati ya watu wa matabaka yote nchini humo.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo leo Jumatano na kumnukuu António Guterres akisema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa Kuijenga Upya Iraq huko nchini Kuwait na kuongeza kuwa, uchaguzi ujao wa Iraq ni muhimu sana katika suala hilo.

Ameongeza kuwa, inabidi kuchukuliwe hatua za maana za kujenga upya mambo yote nchini Iraq ikiwa ni pamoja na mfumo wa elimu, ajira kwa vijana na kuwahudumia akinamama walioathiriwa na mgogoro wa ugaidi nchini Iraq.

Vita vya miaka mingi vimefanya uharibifu mkubwa nchini Iraq

 

Aidha amewataka wajumbe wote walioshiriki kwenye mkutano huo kuzisaidia juhudi za Umoja wa Mataifa katika suala hilo na kusisitiza kuwa, hivi sasa Iraq imefunga milango ya mateso hatari ya huko nyuma na kwamba mkutano huo wa Kuwait umewaletea matumaini wananchi wa Iraq walioathriwa vibaya na masaibu ya kila namna.

Mkutano wa Kimataifa wa Kuijenga Upya Iraq ulifunguliwa siku ya Jumatatu ya tarehe 12 Februari 2018 nchini Kuwait na kuwashirikisha wanaharakati wa sekta mbalimbali zikiwemo za kibenki na kibiashara pamoja na viongozi wa kisiasa kutoka nchi 50 tofauti duniani.

Nchi mbalimbali zimeahidi kuwekeza nchini Iraq kwa mabilioni ya dola kama njia ya kuijenga upya Iraq iliyopitia miaka mingi ya mateso na migogoro.

Tags

Feb 14, 2018 16:40 UTC
Maoni