• Tahadhari ya Sayyid Nasrulah kuhusu njama za Marekani Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa eneo lote la Mashariki ya Kati limekuwa medani ya vita vya mafuta na gesi. Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumzia hitilafu za mpaka wa Lebanon na utawala wa kizayuni wa Israel na mivutano ya pande hizo mbili juu ya vyanzo vya mafuta na gesi katika maji ya pwani ya eneo hilo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ametahadharisha kuhusu duru mpya na njama za utawala ghasibu wa Israel na madola ya kibeberu kama Marekani za kutaka kudhibiti vyanzo vya maliasili ya mafuta na gesi katika nchi za Syria na Lebanon na kusema: Kwa sasa Marekani inasimamia vita vya mafuta na gesi katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Eneo la Mashariki ya Kati siku zote limekuwa mlengwa wa siasa za kibeberu za madola yanayotaka kujitanua na kudhibiti utajiri wa maliasili ya eneo hilo kutokana na nafasi yake ya kistratijia na utajiri wake wa mafuta na gesi. Miongoni mwa siasa hizo chafu za mabeberu ni mpango wa Marekani eti wa Mashariki ya Kati Mpya ambao mhimili wake mkuu ni kudhamini usalama wa utawala haramu wa Israel na kudhibiti utajiri wa nishati wa eneo hilo. Katika fremu hiyo Marekani imeendeleza harakati zake za kijeshi huko Syria na kuna hatari ya majeshi ya nchi hiyo kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo yenye utajiri wa mafuta ya Syria licha ya kuangamizwa kundi la kigaidi la Daesh.

 

Phill Tailor ambaye ni mchambuzi wa masuala ya jiografia ya kisiasa anasema: "Kuendelea kuwepo majeshi ya Marekani nchini Syria ni kwa sababu ya kupora mafuta ya nchi hiyo na kudhibiti njia za kusafirishia bidhaa hiyo, na si kwa sababu za kiusalama pekee." Tailor amesisitiza kuwa: "Tangu awali Marekani ilikuwa na nia ya kutaka kudhibiti utajiri wa mafuta wa Syria na kwamba nchi yoyote isiyokubaliana na matakwa ya viongozi wa Washington hulipa gharama kubwa ikiwa ni pamoja na kutumbukizwa kwenye vita vinavyopiganywa kwa niaba.

Mgogoro uliotokea kati ya nchi kadhaa za Ghuba ya Uajemi pia ambao ulianza baada ya safari iliyoandamana na nuksi ya Donald Trump katika eneo la Mashariki ya Kati pia ulitokana na njama za Marekani na baadhi ya watalawa wa nchi za Kiarabu kwa ajili ya kudhibiti utajiri wa gesi wa Qatar. Ni kwa kutilia maanani hayo yote ndipo ikasemwa kwamba, kwa sasa Marekani inasimamia vita vya mafuta na gesi katika eneo la Mashariki ya Kati. Katika mkondo huo serikali ya Donald Trump inaitambua Iraq kuwa ni "pipa kubwa la mafuta" na kwa msingi huo inataka kudhibiti maeneo yenye utajiri wa mafuta ya nchi hiyo kupitia njia ya kuanzisha kambi mbalimbali za kijeshi nchini humo. 

Donald Trump

Mbinu hiyo hiyo ya Marekani inatumiwa na mwanaharamu wake, yaani utawala ghasibu wa Isarel huko Lebanon ambako imezidisha harakati za kutaka kunyakua maeneo yenye utajiri wa mafuta ya pwani mwa Lebanon. Katika mkondo huo Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel, Avigdor Lieberman, amedai kuwa, eneo la mafuta na gesi la Block 9 huko Lebanon ni milki ya utawala huo. Madai hayo yamepingwa vikali na maafisa wa serikali ya Lebanon. Baada ya hapo na katika safari yake ya hivi karibuni mjini Beirut, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Rex Tillerson aliingilia kati na kutoa pendekezo la kuwa mpatanishi kati ya pande hizo mbili. Inasemekana kwamba, pendekelezo hilo la upatanishi limetegemea vigezo vya Mpango wa "Frederick Hoff" uliobuniwa miaka kadhaa iliyopita. Kwa mujibu wa mpango huo, Marekani imependekeza kwamba, asilimia 60 ya utajiri wa mafuta wa Block 9 iwe mali ya Lebanon na asilimia 40 mali ya Israel. Hata hivyo Walebanon wamekataa mpango huo na kusisitiza kuwa, watasimama kidete dhidi ya njama hizo za Israel na Marekani.      

Tags

Feb 18, 2018 03:12 UTC
Maoni