• Mwaka 2018, mwaka wa kushtadi mgogoro wa kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni

Sambamba na kuongezeka upinzani wa raia wa utawala haramu wa Israel juu ya kuendelea kubakia madarakani Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo kutokana na kuhusika kwake na ufisadi wa fedha za umma, baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vimeelezea kujiandaa Naftali Bennett, Waziri wa Elimu wa Israel na mkuu wa chama cha 'The Jewish Home' kuwa waziri mkuu wa Israel.

Kufuatia ushauri wa polisi ya Israel wa kushtakiwa Netanyahu kutokana na tuhuma za ufisadi na kadhalika kupokea rushwa, viongozi kadhaa wa bunge la Israel Knesset, wamemtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu haraka iwezekanavyo. Ongezeko la mashinikizo pamoja na ukosoaji mkubwa dhidi ya Benjamin Netanyahu katika miezi ya hivi karibuni limekuwa kubwa kiasi cha kuwaathiri hata wajumbe wa muungano wake wa kiutawala. Kwa hakika matukio yanayojiri Israel hivi sasa yanabainisha ongezeko la migogoro ya kisiasa ndani ya utawala huo haramu.

Sambamba na kutolewa mapendekezo kwa ajili ya kuuzuliwa Netanyahu madarakani, navyo vita vya maneno kati ya viongozi wa Israel vimeendelea kupamba moto katika miezi ya hivi karibuni. Kile ambacho hakina shaka ni kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, ulingo wa kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni sasa unaingia katika duru mpya ya tofauti, vita vya kuwania madaraka, migogoro ya kisiasa na kiuchumi, suala ambalo linabainisha kwamba Israel inakabiliwa na wimbi jipya la mizozo ya kisiasa. Utendajikazi uliofeli wa Benjamin Netanyahu hususan katika miezi ya hivi karibuni na unaotajwa kuwa chanzo cha kushadidi migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya Israel, umepelekea kupanuka malalamiko ya raia wa utawala huo dhidi ya viongozi wao katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Ni kutokana na hali hiyo, ndipo weledi wa masuala ya kisiasa wakautaja mwaka 2018, kuwa mwaka wa kushtadi migogoro ndani ya utawala wa Kizayuni. Aidha kushadidi migogoro hiyo ya kisiasa ndani ya Israel kumeenda sambamba na kushindwa mtawalia utawala huo na Intifadha ya Wapalestina, hususan baada ya kushtadi Intifadha ya Quds iliyoshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni. Ongezeko la upinzani dhidi ya Netanyahu na kadhalika kuwepo nyaraka na vielelezo tofauti vinavyoashiria ufisadi wake, yote hayo yanaipa nguvu dhana hii kwamba, umri wa kisiasa wa waziri mkuu huyo wa Israel umekaribia. Katika uwanja huo, mtandao wa intaneti wa gazeti la al-Akhbar la Lebanon umechapisha Makala inayosema kwamba ufisadi wa kiuchumi wa Netanyahu umeyafanya maisha yake ya kisiasa kumulikwa zaidi, na inaonekana kwamba maisha yake ya kisiasa yanaelekea ukingoni.

Viongozi katili wa utawala haramu wa Israel

Aidha suala la Israel kukabiliwa na migogoro chungu nzima, linatia doa mustakbali wa utawala huo bandia. Pamoja na hayo, mauaji ya kila siku dhidi ya raia madhlumu wa Palestina na kadhalika ukatili wa kutisha unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, bado haujakomeshwa. Suala hilo pamoja na mambo mengine linabainisha kwamba watawala wa Israel na vyama vya utawala huo katili, licha ya kuwa na tofauti kubwa baina yao juu ya kuwania madaraka, lakini wote kwa pamoja hawatofautiani hata kidogo juu ya kadhia ya kufanya ukatili na jinai dhidi ya Wapalestina.

Naftali Bennett, Waziri wa Elimu wa utawala haramu wa Israel anayetajwa kumrithi Netanyahu

Jambo jingine ni kwamba ongezeko la tofauti kati ya vyama vya kisiasa ndani ya bunge la utawala huo Knesset, mbali na kuongeza fununu za kuanguka kisiasa Benjamin Netanyahu, linatilia nguvu pia uwezekano wa waziri mkuu huyo kuvunja bunge hilo. Netanyahu alikalia kiti cha uwaziri mkuu wa Israel mwaka 2009 na hadi sasa amekwishavunja bunge mara tatu, na ikiwa atavunja tena bunge hilo kwa mara ya nne, Wazayuni watalazimika kushiriki uchaguzi mpya. Katika mazingira hayo bila shaka utawala wa Kizayuni ambao unakabiliwa na changamoto nyingi za kimataifa, utatumbukia katika changamoto zaidi za ndani.

Tags

Feb 19, 2018 03:03 UTC
Maoni