• Hizbullah yasisitiza tena kwamba, itakabiliana vilivyo na uvamizi wa Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena imesisitiza kwamba, itakabiliana vilivyo na uvamizi wa aina yoyote ile wa utawala haramu wa Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon.

Hayo yameelezwa na Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati hiyo ya Muqawama ambaye amesisitiza kwamba, Hizbullah iko tayari kuisaidia serikali ya nchi hiyo na kutoa majibu kwa uvamizi wa utawala dhalimu wa Israel.

Sheikh Naim Qassim sambamba na kusifu nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mashariki ya Kati amesema kuwa, Israel haina ubavu wa kusababisha madhara kwa haki za baharini na nchi kavu za Lebanon.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon sanjari na kubainisha kwamba, Marekani imejipanga kukabiliana na Iran amesema bayana kuwa, Iran ni muungaji mkono mkuu wa fikra za kimuqawama; na Marekani inataka eneo la Mashariki ya Kati liwe dhaifu, lililogawanywa na linaloiunga mkono Israel.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

Amesisitiza kuwa, kwa kuweko nguvu ya muqawama adui Mzayuni hawezi kufanya uvamizi dhidi ya Lebanon na kupora haki za baharini na nchi kavu za nchi hiyo ya Kiarabu.

Itakumbukwa kuwa, katika wiki za hivi karibuni mivutano kati ya Lebanon na Isreal imeongezeka kutokana na hatua ya Tel Aviv ya kujenga ukuta katika mpaka wa utawala huo ghasibu na Lebanon na madai ya viongozi wa Tel Aviv kuhusiana na eneo la tisa la nishati ya mafuta na gesi la Lebanon. Viongozi wa Lebanon wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, katu hawatalegeza kamba hata kidogo kuhusiana na haki na mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo.

Tags

Feb 20, 2018 04:22 UTC
Maoni